Kufuatia wizara ya afya kutangaza kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya MPOX mnamo tarehe 09 Machi 2025, kamati ya afya ya msingi ya wilaya ya Ilemela imekutana kujadili juu ya namna ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Dkt.Maria Kapinga alitoa elimu ya ugonjwa huo wa homa ya MPOX kwa washiriki wa kikao kwa kuwaeleza chanzo cha ugonjwa huu na dalili zake sambamba na namna ya kujikinga ili kuepukana na ugonjwa huo.
Dkt Maria alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mwili kutokwa na upele/malengelenge, maumivu ya misuli,uchovu wa mwili, maumivu ya mgongo, homa, kuumwa kichwa n.k sambamba na kutaja njia ya kujikinga ikiwemo kuepuka kushikana mikono,kukumbatiana, kunawa mikono na maji tiririka.
Aidha washiriki wa kikao hicho wameombwa kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka juu ya ugonjwa huu na kuhimizwa ushirikiano pindi ambapo itahisiwa kuna mgonjwa kwa kutoa taarifa mapema na sio kuficha ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Pia kupitia kikao hicho mikakati ikawekwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa makundi mbalimbali, kuhakikisha kunakuwepo na maji tirirka katika maeneo mbalimbali kama masoko, stendi za mabasi n.k, usitishaji wa uuzaji wa nyama pori pamoja na upimaji wa hali ya joto kwenye mikusanyiko hususan maeneo ya stendi za mabasi na daladala.
Kikao hicho kilichofanyika tarehe 15 machi 2025 na kuongozwa na wakili Mariam Msengi ambae ni katibu Tawala wa Ilemela akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo kiliwashirikisha viongozi wa dini, wataalam wa manispaa ya Ilemela,viongozi wa makundi ya kijamii kama bodaboda na viongozi wa masoko .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.