Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake ya kimataifa ,Wilaya ya Ilemela imekutanisha makundi mbalimbali ya wanawake kupitia hafla ya Usiku wa mwanamke uliowakutanisha makundi mbalimbali ya wanawake wa Ilemela maalum kwa ajili ya kutambua michango ya wanawake katika jamii ya Ilemela kwa kutoa tuzo za pongezi.
Akikabidhi tuzo kwa wanawake walionyesha kufanya kazi kubwa na kuwa msaada kwa wengine kwa namna tofauti tofauti kwa viwango vya juu Katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela wakili Mariam Msengi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya hiyo amesema ni wakati wa wanawake wote kuungana na kutambua kazi zinazofanywa na wengine ,kuondoa chuki baina yao na kujenga utamaduni wa kusaidiana kufikia malengo waliojiwekea .
“..Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na wanawake katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,malezi katika familia.Wanawake ni jeshi kubwa na tuna nafasi ya kufanya mambo makubwa yenye tija kwa umoja wetu..”
Prisca Mkungu mmiliki wa kampuni ya Jimap Cleaning Services Company Ltd ni miongoni mwa wanawake waliopata tuzo za pongezi kwa kuwa mwanamke jasiri kwa kutoa fursa za ajira kwa wanawake wenzake ambapo zaidi wanawake 15 wameajiriwa kwenye kampuni hiyo.
Wakili Msengi ameongeza kuwa ni wakati wa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea nayo ya kuleta maendeleo kwa kila mwanamke kuitendea haki nafasi aliyo nayo katika jamii huku akianisha uwepo wa miradi mikubwa ya sekta ya elimu,afya na miundo mbinu inayoendelea kutekelezwa Ilemela.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu amesema kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Manispaa yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kufanya shughuli za kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji na kutembelea wagonjwa wa kansa katika hospitali ya Rufaa Bugando huku akiwashukuru wadau hao kwa kufanikisha tendo hilo lenye baraka .
“.. Namshukuru Rais wetu Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua nafasi ya mwanamke kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake,na pia nampongeza kwa kurudisha mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo kwa awamu ya kwanza tayari tumetoa shilingi milioni 618.6 kwa vikundi 39 vya wanawake.Naamini mtarejesha vizuri ili zoezi liwe endelevu na wengine wapate..”
Tumsifu Matutu ni mkazi wa kata ya Kawekamo yeye ni mzungumzaji wa kutia moyo amesema ni muhimu kutambua mipango uliyojiwekea ya kufanikiwa katika maisha na kuwataka kina mama hao kutokuzipa nafasi changamoto za kimaisha kuwazuia kufikia malengo huku akisisitiza upendo baina yao.
Jumla ya tuzo kumi zimetolewa kwa wanawake vinara wanaojishughulisha na ujasiriamali ,biashara na utumishi wa umma.
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.