Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imepongezwa kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za mradi wa green anda smart cities ikiwemo ununuzi wa magari na mitambo ya ujenzi wa barabara, usimikaji wa mifumo katika kituo cha utoaji huduma za kibiashara (ONE STOP CENTER) katika ofisi ya kata ya Nyamanoro na mfumo wa GOT-HOMIS katika zahanati ya Nyamadoke.
Pongezi hizo zimetolewa na Bi Agnetah Rushelya kutoka wizara ya fedha mara baada ya ziara ya kukagua miradi hiyo, ambae amefafanua kuwa kupitia ziara yao wameweza kukagua miradi iliyotekelezwa kwa fedha za mradi wa Green and Smart Cities na kwamba wamejionea namna miradi hiyo ilivyozingatia thamani ya fedha.
“Tumekuja kukagua miradi inayofadhiliwa na Green and Smart Cities, tumeitembelea na tumeona kile kilichofanyika, kwakweli tunamshukuru na kumpongeza mkurugenzi na uongozi wake kwani mradi wa Green and Smart Cities inalenga kuleta tija katika jamii” Alisema Agnetah
Pamoja na pongezi hizo, Bi Agnetah ameahidi kuendelea kushirikiana na manispaa ya Ilemela kupitia mradi wa Green and Smart Cities kwa kuhakikisha miradi mingi inaendelea kutekelezwa na kunufaisha jamii
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu mbali na kuwashukuru wataalam hao kwa kuitembelea manispaa yake, amewataka kuendelea kushirikiana na kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo umaliziaji wa jengo la utawala pamoja na kuahidi kuendelea kusimamia fedha zote zinazoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
Anna Shao ni afisa biashara wa manispaa ya Ilemela anaesimamia kituo cha utoaji huduma za kibiashara katika ofisi ya kata ya Nyamanoro kilichofadhiliwa na mradi huo, amesema kuwa kituo hicho kimesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kwamba huduma za elimu ya biashara, msaada wa kuomba leseni na utoaji wake, huduma za kodi za huduma na ada za nyumba za kulala wageni zinatolewa katika kituo hicho siku zote za kazi kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni
Nae Bi Nadya Daniel ambae ni mfanyabiashara wa kata ya Kitangiri aliyenufaika na uwepo wa kituo cha mlipa mkodi kata ya Nyamanoro kupitia mradi wa Green and Smart Cities ameshukuru kwa uwepo wa kituo hicho kwani kimewasaidia kupata huduma kwa haraka na kwa wakati tofauti na awali ambapo walikuwa wakitumia muda mrefu kufata huduma makao makuu ya wilaya
Ahmed Sakibu ni mratibu wa mradi wa Green and Smart Cities kwa manispaa ya Ilemela amesema kuwa hadi sasa manispaa ya Ilemela imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1.99 kwa ajili ya kutekeleza miradi chini ya programu ya green and smart citIES.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.