Timu ya mpira wa kikapu ya wanaume ya Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imepongezwa kwa ushindi baada ya kuifunga Timu ya halmashauri ya wilaya ya Iringa vikapu 49 kwa 44 katika hatua ya fainali iliyochezwa katika viwanja vya chuo cha ualimu Butimba jijini Mwanza
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo katika uwanja wa mpira wa miguu wa Nyamagana, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe Said Mtanda amesema kuwa mashindano ya shirikisho la michezo serikali za mitaa Tanzania SHIMISEMITA yamekuwa na faida nyingi kwa watumishi ikiwemo kujenga afya, kujenga ukakamavu, weredi, umoja, upendo na mshikamano miongoni mwao sanjari na kuwa Kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza michezo
'.. Nitumie jukwaa hili ninawapongeza watu kutoka Ilemela kwa kupata ushindi katika michezo kadhaa, Mmekuwa mfano mzuri, Mmekuwa wenyeji wema ukilinganisha na wenzenu wa Mwanza jiji ninaamini watajifunza kutoka kwenu ..' Alisema
Aidha Mhe Mtanda amempongeza mwenyekiti wa shirikisho hilo kwa kuleta michezo hiyo mkoa wa Mwanza kwa kuwa Mwanza ndio kitovu cha michezo mbalimbali nchini huku akiwaagiza wakurugenzi kujipanga vizuri kwa mwaka mwengine wa mashindano hayo yatakayofanyika mkoa wa Tanga sanjari na kuwasisitiza wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Kama kauli mbiu ya mashindano hayo inavyosema ya Shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa taifa endelevu
Kwa upande wake nahodha wa Timu ya mpira wa kikapu ya wanaume halmashauri ya manispaa ya Ilemela Ndugu Mponjoli Pheston Basalile amefafanua kuwa mchezo wao dhidi ya Iringa haukuwa mwepesi na kwamba kilichowasaidia kupata ushindi ni makosa madogo madogo ya wapinzani wao pamoja na Timu yake kuzidisha umakini, umoja, kujituma na mshikamano Kama kauli mbiu ya wilaya hiyo inavyosema hivyo kujituma na kuongeza bidii na baadae kupata ushindi huku akiahidi kuendelea kufanya mazoezi zaidi na kujiandaa kwa mwakani ili waendelee kubaki na ushindi huo kwa siku zijazo
Nae afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Mwalimu Kizito Bahati Sosho akafafanua kuwa mchezo wa mpira wa kikapu haukuwahi kuwepo tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo nakwamba manispaa ya Ilemela inakuwa ya kwanza kushinda kipengele hicho huku akiongeza kuwa hata katika michezo mengine manispaa yake ilikuwa ikifanya vizuri isipokuwa makosa madogo madogo ndio yaliyowafanya wakakosa ushindi na kwamba watajirekebisha ili wafanye vizuri katika mwaka mwengine huku akimshukuru mkurugenzi wa Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu kwa kuunga mkono Timu yao kuanzia mwanzo mpaka tamati ya mashindano hayo
Mashindano ya shirikisho la michezo serikali za mitaa Tanzania SHIMISEMITA yalianza mapema Agosti 25, na kufikia tamati Leo hii Septemba 05, ambapo halmashauri mia moja zimeshiriki zikichuana kupata mshindi wa michezo mbalimbali ikiwemo bao, karata, mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, kuvuta kamba, pool table na mpira wa mikono
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.