Manispaa ya Ilemela imepongezwa kwa kukamilisha maandalizi ya mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa uliozingatia kikamilifu mfumo wa usimamizi wa maafa nchini uliowekwa na sera ya taifa ya menejimenti ya maafa ya mwaka 2004 na sheria ya usimamizi wa maafa namba 6 ya mwaka 2022
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa wataalam wa timu za utayari za kukabiliana na maafa kwa Wilaya ya Ilemela ambayo yatachukua takriban siku tatu ambapo serikali inashirikiana na taasisi ya IOM UN-MIGRATION.
Sambamba na pongezi hizo ameendelea kusema kuwa yapo majanga mbalimbali kama ya moto, mafuriko, ajali za vyombo vya usafiri na magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakitokea, hivyo mpango huo utasaidia uwajibikaji wa kila sekta na idara pamoja na ushirikiano wa wadau katika kukabiliana na maafa
“Nawapongeza Ilemela kukamilisha mpango wa kukabiliana na maafa, Hii itasaidia ikitokea changamoto ya moto jamii ya eneo husika itajua namna ya kutumia vifaa vya moto”, Amesema
Aidha Meja Mbuge amewataka wadau kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na majanga pamoja na kuimarisha mfumo wa mawasiliano muda wote kwa kupitia utaratibu uliopo
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary mbali na kuishukuru Serikali kwa kuwajengea uwezo wataalam wake amemuhakikisha mkurugenzi huyo wa majanga juu ya utekelezaji wa ushauri uliotolewa katika kukabiliana na maafa au majanga
Nae Ndugu Charles Msangi kutoka idara ya menejimenti ya maafa ofisi ya waziri mkuu amefafanua kuwa matukio yanapotokea timu za maafa ndio zinatakiwa kuwa za kwanza kuwajibika ili kuweka utayari na kupunguza madhara kwa kuwa maafa hayana mfumo mpya
Afisa Uhasibu wa manispaa ya Ilemela ambae ni mjumbe wa kamati ya maafa na majanga Bi Nongwa Idilia Gilbert ameshukuru kwa mafunzo yaliyotolewa na kwamba yatasaidia jamii katika kukabiliana na maafa au majanga yatakayojitokeza
Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.