Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imepokea msaada wa vitanda kumi vya kisasa vitakavyotumika kwenye wodi ya wazazi ya kituo cha afya cha Buzuruga vyenye jumla ya thamani ya kiasi cha dola za kimarekani elfu nne sawa na shilingi za kitanzania milioni tisa na laki tano kutoka kwa shirika la maendeleo la watu wa Korea (KOICA) kwa kushirikiana na jumuiya ya wanafunzi waliosoma nchini humo inayojulikana kama KOAT
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya kituo cha afya Buzuruga, Mwakilishi mkazi wa shirika la Korea nchini (KOICA) Bwana Manshik Shin mbali na kuishukuru jumuiya ya watu waliosoma Korea kwa kuratibu tukio hilo amesema kuwa anatambua changamoto zinazoikabili nchi ya Tanzania na kwamba Serikali ya Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu hivyo kinachofanyika sasa ni moja ya utatuzi wa kero hizo
‘.. Niombe uongozi wa kituo cha afya Buzuruga na manispaa ya Ilemela kwa ujumla wake kupokea mchango wetu, Mchango huu umetoka kwa watu wa Korea na Serikali yao kwa lengo la kutatua changamoto za wananchi kama sehemu ya ushirikiano wetu ..’ Alisema
Aidha Bwana Shin ameongeza kuwa msaada uliotolewa utaenda kupunguza changamoto zilizokuwepo japo kwa uchache huku akiahidi kuendelea kuona namna bora ya kushirikiana katika kumaliza kero zilizobaki zinazokabili wananchi
Kwa upande wake Rais wa jumuiya ya wanafunzi waliosoma nchini Korea (KOAT) Dkt Deman Abdi Yusuf amefafanua kuwa wamekuwa wakishirikiana na shirika la KOICA kutoa msaada katika nyanja mbalimbali zenye uhitaji nchini huku akitolea mfano msaada kama huo uliotolewa katika kituo cha afya Kurasini, ujenzi wa kituo cha damu salama cha kisasa jijini Dodoma, hospitali ya Muhimbili tawi la Mloganzila hivyo kuwaalika wa Tanzania kujiunga na jumuiya hiyo kwa kuwa inagusa maisha ya wengi na nchi kwa ujumla
Nae mganga mkuu wa kituo cha afya Buzuruga Daktari William Tinginya amesema kuwa licha ya kituo hicho kuhudumia wananchi wengi mpaka wa kutoka nje ya wilaya bado kinakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba ikiwemo vitanda 32 licha ya leo kupokea vitanda 10, upungufu wa watoa huduma za afya wakiwemo madaktari, manesi na wataalam wengine wa afya hivyo kuomba shirika hilo na wadau wengine kuendelea kuona namna bora ya kukisaidia kituo hicho ili kiendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akitoa neno la shukrani Mstahiki Meya Wa Manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga mbali na kuwapongeza wadau hao wa maendeleo, amewahakikishia ushirikiano kutoka katika manispaa anayoiongoza na kwamba Serikali peke yake haiwezi kumaliza changamoto zote zinazokabili wananchi bila ushirikiano kutoka kwa wadau wengine wa maendeleo
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.