Katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela Adv.Mariam Msengi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Hassan Masala amepokea jumla ya madawati 170 yenye thamani ya takriban shilingi millioni 11.9 na miti 1700 kutoka kwa mdau wa maendeleo taasisi isiyo ya kiserikali ya Desk & Chair Foundation.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi hayo Adv.Msengi amesema madawati hayo yamekuja kwa wakati muafaka kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati uliopo katika baadhi ya shule ndani ya Manispaa ya Ilemela.
"Tunashukuru sana kwa msaada huu kwani inaonyesha tupo pamoja na serikali ya awamu ya sita katika kuindeleza sekta ya elimu ,wote ni mashahidi kwa fedha nyingi zinazoendelea kuletwa na Mhe.Rais za miradi ya Boost na Sequip kwa ajili maboresho katika shule zetu."
Aidha Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sibtain Meghjee ametoa taarifa ya utendaji kazi huku akisisitiza utaratibu wao wa kuhamasisha jamii utunzaji wa mazingira kwa kutambua kuwa utengenezaji wa madawati unatumia miti hivyo ni lazima miti ipandwe kwa wingi zaidi kwa kuwa bado vizazi vinaendelea.
" Ni utaratibu wetu kila tunapotoa madawati ni lazima tupande mingine,kila dawati tunatoa miti 10.Hii ni kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo."
Nae Mwenyekiti wa kamati ya huduma za uchumi ,afya na elimu wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Hussein Magela diwani wa kata Ibungilo kwa niaba ya mstahiki Meya wa Manispaa hiyo amewapongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri wanazofanya za kusaidia jamii.
"Kwa sisi tunaoamini Mungu kazi hii mnayoifanya ni ya kumcha Mungu, watoto wetu watasoma vizuri mafanikio yao sio yao tu bali ni ya jamii nzima."
Mwakilishi wa madiwani wa Manispaa hiyo diwani wa kata ya Kitangiri Mhe.Donald Ndalo amesifu utaratibu wa taasisi ya desk and chair foundation kuona mbali zaidi kwa kutoa madawati na miti kwa maana ya kuongeza miti zaidi .
Leah Cosmas ni mwanafunzi katika shule ya msingi Kaserya yeye anashukuru kwa madawati hayo na kuahidi ufaulu mzuri.
Akihitimisha hafla hiyo kaimu Mkurugenzi wa Manispaa Mwl.Marco Busungu amewataka waalimu wote wa shule za msingi waliokabidhiwa madawati hayo kuyatunza na maeneo yote miti inakoenda kupandwa kusimamiwa vizuri isiharibiwe na tija yake ikaonekane .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.