Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela limefanya uchaguzi na kupata naibu mstahiki meya kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Akizungumza mara baada ya zoezi la uchaguzi wa naibu meya na wenyeviti wa kamati za kudumu, Mstahiki meya wa manispaa hiyo Mhe. Renatus Bahebe Mulunga amempongeza diwani wa kata ya Buzuruga Mhe. Manusura Sadick Lusigaliye kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo kwa awamu nyingine huku akiwakata madiwani wenzake kuungana mkono na kupendana ili shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa hiyo ziweze kufanikiwa na kuyafikia malengo ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan .
‘.. Nakupongeza sana naibu meya lakini pia niwaombe waheshimiwa madiwani Mwenyezi Mungu anapenda mshikamano na kupendana tukishirikiana vya kutosha tutamaliza kwa amani kama kauli mbiu yetu inavyosema Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ..’ Alisema
Aidha Mhe. Mulunga amewataka madiwani kuendelea kusimamia fedha za miradi ya maendeleo zinazoletwa katika maeneo yao huku akimshukuru Mbunge wa jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula kwa kuwa kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa hiyo.
Kwa upande wake naibu meya wa Manispaa ambae pia ni diwani wa kata ya Buzuruga Mhe.Manusura Sadick Lusigaliye mbali na kulishukuru baraza la madiwani kwa kumuamini na kumchagua tena amewahakikishia ushirikiano madiwani wenzake pamoja na kuahidi kusimamia fedha zote za maendeleo zitakazoletwa na Serikali kuu pamoja na zile za mapato ya ndani.
Nae Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt. Angeline Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo alizozitoa kwa Jimbo la Ilemela sanjari na kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi. Ummy Mohamed Wayayu kwa kazi nzuri anazozifanya .
Yusuph Ernest Bujiku ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela amewataka madiwani hao kushirikiana ili ilani ya uchaguzi na shughuli za maendeleo ziweze kusonga pamoja na kusisitiza kuwa chama hakitamvumilia diwani yeyote anaekwamisha jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi .
Donard Ndaro diwani wa kata ya Kitangiri amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za uchumi, afya na Elimu, Godlisten Kisanga diwani wa kata ya Mecco amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya mipango miji, ujenzi na mazingira, wakati Kamati ya ukimwi ikiongozwa na naibu meya Manusura Sadick Lusigaliye na Kamati ya fedha ikiongozwa na mstahiki meya Mhe Renatus Bahebe Mulunga.
|
|
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.