ILEMELA YAJIPANGA KUTEKELEZA VYEMA ZOEZI LA UGAWAJI WA VITAMBULISHO KWA WAJASIRIAMALI
Katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli, linalohusu ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, Baraza la Madiwani la Manispaa ya Ilemela chini ya Mstahiki Meya, Mhe. Renatus Mulunga limeridhia mapendekezo ya utaratibu wa utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara hao.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa na mratibu wa sekta isiyo rasmi Ilemela, Ndugu Raphael Mphuru,ambapo aliyataja kuwa ni pamoja na, kutenga kanda zitakazohusika katika zoezi, uundaji wa kamati maalum ya kusimamia zoezi la ugawaji wa vitambulisho, uundaji wa kamati za kuratibu vitambulisho vya wamachinga za kanda pamoja na kutengeneza kanzi data.
John Wanga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela amesema kuwa lengo ni kuhakikisha zoezi linafanikiwa kwa mafanikio makubwa ili halmashauri iweze kuwa ya mfano nchini kwa kutekeleza vyema zoezi la ugawaji wa vitabulisho vya wajasiriamali wadogo.
“Ili kufanikisha zoezi hili, tumezishirikisha taasisi za I4ID na Kivulini kwa vile ni taasisi ambazo tumekuwa tukifanya nazo kazi kwa karibu na hapo awali kabla ya tamko la Mhe.Rais walikuwa wameanza utafiti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wajasiriamali wadogowadogo” , alisema
Pamoja na hayo alisema kuwa vitambulisho hivi vitalipiwa kiasi cha Shilingi za kitanzania elfu ishirini (Tshs.20,000) fedha ambazo baada ya kukusanywa itawekwa kwenye akaunti ya kamishna wa kodi za ndani kwenye benki zilizoidhinsihwa kukusanya mapato.
Mbunge wa Ilemela, Mhe. Angeline Mabula alishauri kuwa zoezi hili lisiingiliwe na wanasiasa ili kuleta ufanisi bali wawe sehemu ya kutoa ushauri pale ambapo zoezi litakuwa haliendi sawa, aidha alisistiza kuwa makini katika kuyatambua makundi mbalimbali kuwepo na uwiano sawa ili kuweza kuwagusa wote kwa pamoja bila kulisahau kundi la walemavu.
Halikadhalika alisisitiza kuwa watakaopewa vitambulisho hivi, ni wale ambao wapo katika maeneo rasmi yaliyotengwa na serikali na si vinginevyo.
Manispaa ya Ilemela itazindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali siku ya tarehe 27/12/2018 katika soko la Kiloleli kata ya Nyasaka.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.