“Asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hatashukuru, suala hili sio dogo ni kubwa nimefurahishwa sana na msaada huu.”
Ni kauli iliyotolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe. Renatus Mulunga wakati akipokea msaada wa thamani ya Shilingi Milioni 1.03 kutoka RUDEA ambacho ni Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Kijamii
Aidha Mhe Mulunga amemtaka Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo ya Nyamadoke kuhakikisha wanatumia vifaa na fedha zilizotolewa kwa uadilifu mkubwa ili kukidhi malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma katika zahanati hiyo
Chama hicho cha RUDEA SACCOS LTD chenye namba za usajili (REG.NO.PR-MZA-ILE-MC-2022-2393) kimetoa msaada wa thamani ya Shilingi Milioni 1.03 fedha za kitanzania kwa zahanati ya Nyamadoke katika kata ya Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya marekebisho katika maabara katika zahanati hiyo ambapo wametoa vifaa vya ujenzi vya thamani ya Tshs. 738,500 sambamba na pesa taslim kwa ajili ya ujenzi Tshs.300,000.
Akisoma taarifa kabla ya kukabidhi msaada huo, Bi Magdalena Lwinga ambae ni Mwenyekiti wa RUDEA SACCOS amesema kuwa walitenga fedha hiyo kwa ajili ya kuhudumia jamii hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 80(1) cha sheria ya vyama vya Ushirika no 6 ya mwaka 2013 ikisomwa sambamba na kanuni ya 55 (c) ya kanuni ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo ya mwaka 2015.
Nae Kaimu Mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Mwanza Ndugu Leo Zephania amewashukuru na kuwapongeza RUDEA SACCOS kwa maamuzi waliyofikia na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa msingi wa saba wa ushirika unaosema kuijali jamii
“Ushirika ni sehemu ya jamii kwa sababu tunafanya kazi na jamii hivyo tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba kile kidogo tunachokipata tunakirudisha kwenye jamii ambayo na sisi tunatoka na ndio tunaofanya nao kazi kwani hicho kidogo kimepatikana kutokana na jamii husika”,Amesema Ndugu Leo
Diwani wa Kata ya Nyamhongolo Mhe Nginila nae amewashukuru wana RUDEA SACCOS kwa msaada huo na kuwaomba kuendelea kuifikiria zahanati hiyo ya Nyamadoke kwani bado inayo mahitaji mengi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.