ILEMELA YAENDELEA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI WA ARDHI
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mheshimiwa William Lukuvi alilolitoa mapema Septemba,2017 la kuhakikisha kuwa manispaa inashirikisha wananchi katika upimaji wa maeneo ya taasisi na kuilinda mipaka ya maeneo hayo.
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mheshimiwa Daktari Leonard Masale amewataka viongozi wa mitaa kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa ardhi sambamba na kusisitiza juu ya utendaji wa haki katika zoezi hilo kwa kuzingatia maelekezo ya waziri wa ardhi Viongozi wenzangu wa mitaa niwaombe mkatoe ushirikiano kwa wataalamu wetu wanapokuja maeneo yenu mkumbuke kuwa wote tuna ajenda ya pamoja,
Tukahakikishe usalama wao na kuwaelemisha wananchi wetu pale inapotokea sintofahamu ya namna yeyote ile na wataalamu niwaombe mkatende haki kwa kuzingatia maelekezo ya mheshimiwa waziri wa ardhi , sheria na taratibu”, Alisisitiza hayo katika kikao kilichoketi kwa ajili ya kuandaa utaratibu bora wa kumilikishwa viwanja hivyo baada ya zoezi la upimaji.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ndugu John Wanga kupitia kikao hicho ameisisitiza timu ya wataalamu inayoendelea kuongeza juhudi ili kuweza kukamilisha zoezi hilo huku akiwataka viongozi wa mitaa kusaidia serikali katika kuyalinda maeneo yote ya umma yasivamiwe.
Kwa upande wao wenyeviti wa mitaa hiyo na wazee mashuhuri wamemuhakikishia mkuu wa wilaya na mkurugenzi ushirikiano kwa wataalamu wanaoendelea na zoezi hilo na kuhakikisha wanayalinda maeneo ya umma yasivamiwe.
Nae afisa mipango miji ndugu Francis Mwanga amebainisha hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuhakikisha maeneo ya taasisi yanainishwa, kupimwa, kumilikishwa na kulindwa ikiwemo kuunda kamati ambayo imeshirikiana na kitengo cha mipango miji kuandaa mpango wa maeneo, kutambua maendelezo ili kuyajumuisha katika mchoro wa mipango miji, kuandaa mchoro wa mipango miji unaojumuisha maeneo ya taasisi, kuidhinisha mpango katika ngazi zote, kufanya upimaji wa mpango, kufanya ukaguzi wa viwanja na baadae kumilikishwa.
Kikao hicho kilijumuisha watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi , wataalamu wa ardhi wa Manispaa , ofisi ya ardhi kanda ya ziwa, wazee mashuhuri na viongozi wa mitaa ya Bwiru Elimu na Bwiru Ziwani.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.