Katika kipindi cha miaka mitano mfululizo halmashauri ya manispaa ya Ilemela imeendelea kupata hati safi (unqualified opinion), hayo yamesemwa na ndugu Athuman Mustapha mkaguzi mkuu wa nje alipowasilisha taarifa ya hesabu zilizokaguliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye mkutano maalum wa baraza la madiwani uliofanyika tarehe 26 Juni 2024 ukihudhuriwa na Mkuu Wa Mkoa Wa Mwanza Mhe. Said Mtanda.
Akiwasilisha taarifa hiyo Ndugu Mustapha amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 hoja 17 zimetekelezwa huku hoja saba zikiwa katika hatua za utekelezaji ambapo amezitaja baadhi ya sababu ya kutofutwa kwa hoja hizo ni kukosekana kwa baadhi ya vielelezo.
Nae Mhe Said Mtanda Mkuu Wa Mkoa Wa Mwanza, akizungumza na baraza la madiwani, ametumia nafasi hiyo kuipongeza Manispaa ya Ilemela kwa kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo huku akimtaka mkurugenzi kuhakikisha anazifuta hoja zilizobakia ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mpango kazi wa kujibu hoja zilizobaki katika ofisi ya Mkuu Wa Mkoa kupitia katibu tawala ifikapo tarehe 28 juni 2024.
“Pongezi nyingi kwa Manispaa ya Ilemela, kwa kuendelea kupata hati inayoridhisha (hati safi) kwa miaka mitano mfululizo, nyie mkipata hati safi maana yake msimamizi wa halmashauri ambae ni mkuu wa mkoa nae amefanya kazi nzuri”amesema mhe mtanda.
Aidha Mhe Mtanda ameutaka uongozi wa Ilemela kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa hesabu za mwaka 2023/2024 ili kuweza kushughulikia hoja hizi kwa wakati na kuweza kufuta hoja zote
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga kwa niaba ya baraza la madiwani amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo aliyoyatoa na kumuahidi kuendelea kuwasimamia watendaji na kuhakikisha kuwa hoja zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati.
Kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa (local government finance act 1982) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, kila baada ya mwaka wa fedha kuisha halmashauri zinapaswa kuwasilisha taarifa zake za hesabu kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa ajili ya ukaguzi na baada ya ukaguzi halmashauri hupewa nafasi ya kujibu hoja
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.