Katika jitihada za kutokomeza utapiamlo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia kitengo cha lishe imeanzisha zoezi la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wenye utapiamlo mkali katika mitaa yote 171 inayounda Manispaa hiyo
Hilo limedhihirika katika zoezi la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wanaoishi katika Manispaa ya Ilemela lililongozwa na Bi Mariam Msengi ambae ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela.katika Kituo cha Afya cha Buswelu.
Akikabidhi chakula hicho kwa wazazi wa watoto hao, Bi Mariam Msengi ambae alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, amesema kuwa Manispaa ya Ilemela inaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za uboreshaji wa huduma za lishe kwa kutoa fedha katika sekta hiyo kwa kutambua umuhimu wa wananchi wote kuwa na lishe bora tangu wakiwa wadogo ili kuwa na nguvu kazi imara katika ujenzi wa taifa letu.
Sambamba na hilo Bi Mariam, amewapongeza wakina baba waliofika katika kituo cha afya Buswelu kwa ajili ya kupata huduma za kliniki pamoja na kusikiliza elimu ya lishe huku akiwasihi kina baba waliopo nyumbani kuhamasika na kutenga muda wa kuwa na watoto wao.
" Nawapongeza kina baba waliojitokeza hapa leo kuleta watoto wao kupata huduma za kliniki na pia kusikiliza elimu ya lishe inayotolewa na wataalam ni kitu kizuri na kinajenga upendo wa mtoto kwa wazazi wote wawili baba na mama.Kina baba wengine huko nyumbani mhamasike kutenga muda wa kuwa na watoto wenu kama hivi ."
Nae mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilemela Bi.Nyabwire Lukumai amesema kuwa Manispaa ya Ilemela kupitia idara ya afya inaendelea kuhamasisha ushiriki wa kina baba katika huduma mbalimbali za uzazi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto wao kliniki.
" Mtoto ni wa wote hivyo kwa pamoja baba na mama wanawajibika katika malezi katika nyanja zote." Amesema Bi.Nyabwire
Akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe Ilemela Bi.Pili Kassim amesema Halmashauri imeendelea kutenga kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 katika kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kwa lengo la kupunguza na kutokomeza utapiamlo na kuendelea kuhamasisha jamii kulima mazao yenye viini lishe kwa wingi ili kuimarisha afya zao.
Bwana na Bibi Nzobana ni wakazi wa kata ya Kahama katika mtaa wa Buyombe wao wanaipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa ugawaji lishe sambamaba na utoaji wa elimu endelevu ya lishe kwa wananchi.
Nae Juma Alphonce ni mzazi wa Judith yeye ni mkazi wa kata ya Shibula anajivunia kuwa baba bora kwa kutoa huduma mbalimbali zinazohitajika kwa mwanae.
Kiasi cha Shilingi Milioni 7.45 kimetumika kununua chakula lishe hicho ambacho kimetolewa kwa watoto 40 wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka 5 wenye utapiamlo mkali ambapo lengo ikiwa ni kuwafikia watoto 100 kwa kila robo ya mwaka
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.