Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeanza kutekeleza zoezi la uthamini kwa wananchi wake wa mitaa ya Lukobe na Buduku kata ya Kahama waliokuwa wanaishi katika mipaka ya Jeshi la wananchi wa Tanzania na kusababisha mgogoro mkubwa na wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka kumi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kuthaminiwa, Naibu waziri wa Wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ambae pia ni mbunge wa jimbo la Ilemela, Mheshimiwa Daktari Angeline Mabula amewatoa hofu wananchi hao pamoja na kuwataka kutolihusisha zoezi hilo na siasa kwa kuhakikisha wanakuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na Manispaa ili kuongeza ufanisi na kulifanikisha zoezi hilo kwa wakati na haki ili kila mmoja aweze kupata stahiki yake.
‘.. Niwaombe kuwa wavumilivu kwa masuala yote yenye uhitaji wa kisheria na yale ya maridhiano kati ya pande mbili, Hakuna mwananchi atakaepunjika, hakuna mwananchi atakaedhulumika na hakuna mwananchi mwenye haki atakaeachwa kikubwa kinachotakiwa ni kutoa ushirikiano ..’ Alisema
Aidha Daktari Mabula mbali na kuwashauri wananchi hao juu ya kufungua akaunti za Benki ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano chini Rais Mhe Daktari John Magufuli kwa kusaidia wananchi wanyonge na Viongozi wa Wizara ya Ulinzi kwa kulipa kipaumbele jambo hilo kwa kutenga Bilioni 16 kwa migogoro yote ya ardhi nchi nzima huku Bilioni 3 na milioni 534 zikipelekwa mtaa wa Nyagungulu kata ya Ilemela kuanza kulipa fidia wananchi wa mtaa huo baada ya kuisha kwa zoezi la uthamini na uhakiki.
Kwa upande wake kiongozi wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Ulinzi, Luteni Kanali Mgugule amesema kuwa lengo la zoezi ni kuwafidia wananchi ili kupisha eneo la jeshi kwa sababu za kiusalama na kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima sambamba na kuwashukuru kwa kupokea vizuri zoezi hilo huku akiwahakikishia kutenda haki na kuwataka kuliamini jeshi lao.
Mwenyekiti wa mtaa wa Lukobe, Ndugu Paul Lameck ameishukuru Serikali na mbunge wa jimbo hilo kwa juhudi kubwa alizozichukua kuhakikisha wananchi wake wanapata fidia na kuumaliza kabisa mgogoro huo uliokuwa ukiwatesa kwa miaka mingi huku akiahidi kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo.
Kennedy Chiguru ambae ni Afisa Mipangomiji kutoka manispaa ya Ilemela alisema kuwa Zoezi hili la uthamini ni la muda wa kipindi cha siku saba yaani kuanzia tarehe 1-7 mwezi julai hivyo kuwataka wananchi kujitokeza katika maeneo yao na kutoa taarifa sahihi ili kupunguza changamoto zisizo za lazima.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.