Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeanza maandalizi ya zoezi la kampeni ya utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Surua, Polio na Rubella kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Zoezi hilo la utoaji wa chanjo litafanyika mwezi Oktoba kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 15-19/10/2019 ambapo litaendeshwa kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 hata kama walishapata chanjo hiyo kwa utaratibu wa kawaida.
Akifungua kikao cha maandalizi cha kamati ya afya cha Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ambae ndie Mwenyekiti wa kamati hii, Mhe Dkt Severine Lalika amewataka wajumbe wa kamati hiyo ya afya kuhakikisha wanatimiza jukumu lao la msingi la kuunga mkono Sera za Serikali juu ya masuala ya afya ili kuhakikisha wananchi wa wilaya hii wanakuwa salama na kuendelea na utekelezaji wa shughuli zao kila siku za maendeleo
“Tunayo dhamana kuhakikisha tunalisimamia zoezi la afya kiujumla kwani huwezi ukawa na maendeleo ukiwa na watu wenye udhoofu wa afya. Huku tukiamini kuwa mtoto anatakiwa akue akiwa na afya nzuri ili baadae aje awe kiongozi bora kwa taifa letu”, alisisitiza
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela John Wanga amewataka watoa huduma za afya kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa umakini na uaminifu mkubwa huku akisisitiza kufanyika kwa maandalizi ya uhakika.
Nae mratibu wa chanjo wilaya ya Ilemela Bi Veronica Masawe amesema kuwa ni asilimia 85 tu ya watoto wanaozaliwa ndio hupata chanjo, hivyo zoezi hili litakwenda kuziba pengo la 15% inayobaki ya watoto wanaokosa chanjo huku akisisitiza kuwa Chanjo hizi ni salama na zimethibitishwa na shirika la Afya ulimwenguni na Wizara ya afya
Manispaa ya Ilemela inatarajiwa kuzindua kampeni hiyo katika kituo cha afya Buzuruga kilichopo kata ya Buzuruga.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.