Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na shirika la USAID kupitia mradi wake wa afya yangu mama na mtoto wameungana katika mitaa 10 kwa ajili ya utekelezaji wa maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa yanayoadhimishwa na Halmashauri hiyo kila robo ya mwaka.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu ya lishe bora kwenye viwanja vya shule ya msingi Chasubi iliyopo kata ya Kayenze Afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasimu amesema maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIM) hujumuisha huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma za chanjo,wajawazito,matibabu ya watu wazima na watoto,elimu ya uzazi wa mpango ,ushauri wa lishe sambamba na jiko darasa.
"...natamani wote hapa muelewe umuhimu wa lishe bora kwa familia zetu."
Nae mwenyekiti wa mtaa wa Lutongo Daud Malaji amesema taifa letu linahitaji watu wenye afya njema kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika nyanja mbalimbali jambo linalotokana na ulaji wa lishe bora kwa kipindi chote cha makuzi huku akiwasihi wananchi kuchukulia suala la lishe kwa umuhimu mkubwa.
Aidha elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza imetolewa na msisitizo kwa kina mama wote wenye watoto wachanga kunyonyesha ipasavyo.
Helena Shija ni mkazi wa mtaa wa Lutongo yeye anashukuru kwa darasa la mapishi kwa ajili ya maandalizi ya chakula cha watoto chenye viinilishe vyote muhimu.
" Hii lishe ni nzuri mimi huwa nawapa wanangu vyakula hivi kwa mchanganyo wa makundi yote ya vyakula na wana afya nzuri sana."
Maadhimisho hayo ya SALIM yanaendelea kwa mitaa yote 171 inayounda Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.