Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Kampuni ya STECOL Corporation Ltd leo tarehe 17/07/2019 imetiliana saini mkataba wa miradi miwili ya kimkakati ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi pamoja na ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo.
Ujenzi huo wa kituo cha kisasa cha mabasi pamoja na ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo utafanyika katika eneo la nyamhongolo na unatarajia kuanza mnamo tarehe 30/7/2019 na unatarajia kukamilika ndani ya miezi 18.
Miradi hii yote miwili inatarajia kugharimu takribani kiasi cha Shilingi Bil.27 za kitanzania ambapo mradi wa kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi kitagharimu kiasi cha Shilingi 18,719,058,426.19 na ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo itagharimu kiasi cha shilingi 8,376,045,038.21.
Akiongea mara baada ya zoezi la utiaji saini kukamilika Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga amesema kuwa anaamini kuwa kazi hii itafanyika kwa uadilifu na kwa wakati uliopangwa ili ulete tija kwa wananchi wa Ilemela.
Nae Mwakilishi wa kampuni ya STECOL Bwana Luo ameishukuru Manispaa ya Ilemela kwa kuwaamini na kuwachagua kutekeleza mradi huu huku akiahidi kuwa watahakikisha kuwa wanafanya kazi kwa uadilifu na kukamilisha ndani ya miezi 18 iliyokubalika katika mkataba.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Paul John Wanga amemshukuru Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt John Pombe Magufuli, kwa kuipatia Manispaa ya Ilemela fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hii mikubwa ya kimkakati ambayo itawaletea maendeleo wananchi wa Ilemela.
Miradi hii miwili ni kati ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na halmashauri mbalimbali nchini na kufadhiliwa na serikali kuu na lengo kubwa ikiwa nikuhakikisha kuwa Halmashauri inaongeza vyanzo vya mapato ili ziweze kujitegemea.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.