Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imekusudia kuzitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji kupitia mfumo wa ubia (PPP) lengo ikiwa ni kuongeza ubora na ufanisi wa utoaji huduma pamoja na kupanua wigo wa vyanzo mbadala vya bajeti ya serikali.
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Wayayu alipokuwa akiwasilisha mapendekezo hayo mbele ya baraza la madiwani la robo ya kwanza 2024/2025 lililofanyika siku ya 06 novemba 2024.
“Mpango huu wa uwekezaji utatekelezwa kwa kuzingatia sera ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi yaani (PPP)”, alisema Ummy
Aidha aliendelea kufafanua kuwa kupitia sheria ya PPP sura ya 103 na kanuni za PPP za mwaka 202 imeweka utaratibu wa kuongeza ubora na ufanisi wa huduma pamoja na kupanua wigo wa vyanzo mbadala vya bajeti ya serikali ili kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kushirikisha sekta binafsi.
Baraza la madiwani wakichangia mapendekezo hayo, walimpongeza mkurugenzi pamoja na timu ya wataalam kwa kuja na mawazo hayo kwa maendeleo ya Ilemela huku wakishauri timu ya wataalam kuhakikisha wanayatambua maeneo yote ya wazi ya Ilemela yatambuliwe ili kuweza kunufaika nayo
Maeneo ambayo yanakusudiwa kutangazwa kama fursa za uwekezaji ni pamoja na eneo la uwekezaji Kirumba, eneo la soko la Nyasaka, eneo jingine ni soko la zamani la Nyamanoro, stendi ya zamani ya mabasi ya Buzuruga, eneo la stendi ya daladala Buswelu, pamoja na maeneo yite ya Buffer zone.
Ndugu Herbet Bilia ambae ni mchumi wa manispaa ya Ilemela, alifafanua kuwa, maeneo hayo yaliyopendekezwa yanafaa kwa ajili ya uwekezaji wa kujenga nyumba za kupangisha, kwa ajili ya kujenga kumbi za kisasa,biashara mbalimbali kama vile michezo ya Watoto, ‘Car Wash’, bustani, sehemu za mapumziko na burudani mbalimbali sambamba na ujenzi wa hoteli na ujenzi wa kitega Uchumi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.