Dhima kuu ya mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia (2024-2034) uliozinduliwa mwezi Mei 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, endelevu, salama na rahisi kutumika,ukilenga kutoa mwongozo wa namna ya kupunguza athari za kiafya, mazingira na kuboresha maisha ya wananchi huku ukipunguza athari ya mabadiliko ya tabia nchi
"Awali tulikuwa tunaumwa vifua, macho, mafua kutokana na moshi wa kuni lakini kwa sasa kutokana na nishati hii mbadala mazingira ni masafi hakuna tena moshi hivyo wanafunzi nao watarajie chakula kisafi kitaiva kwa wakati",anasema Amos Stanley
Amos stanley ni mpishi wa shule ya sekondari Buswelu, ameshukuru kwa mradi wa nishati safi ambao umefanikisha kufanya kazi katika hali ya usafi na usalama , chakula kinaiva vizuri na kwa wakati.
Nao wanafunzi wa Buswelu Sekondari wameshukuru kwa nishati hii mbadala kwani imewasaidia wao kuwahi masomo kutokana na kwamba chakula kinaiva kwa wakati kufuatia uwepo wa jiko hili la nishati safi hivyo wameishukuru serikali kwa kampeni hii ambayo pia inasaidia utunzaji wa mazingira
"Zamani wapishi walikuwa wanachukua muda mrefu kupika kwa sababu ya matumizi ya kuni hivyo kuwapelekea kuchelewa masomo yao, lakini sasa kufuatia uwepo wa nishati mbadala inasaidia, nishati mbadala imesaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira, nishati mbadala imetusaidia kuweka mazingira katika hali ya usafi na salama"
Akizindua huduma hiyo ya matumizi ya nishati safi katika shule ya sekondari Buswelu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Ismail Ussi amepongeza Wilaya kwa jitihada za kuhakikisha matarajio ya Mhe Rais yanafikiwa
"Kufuatia matumizi ya nishati safi tunaona kuwa jengo limetumika lakini bado ni safi hii ni kwa sababu ya nishati safi ambayo tunatumia, ambayo imesaidia juu ya utunzaji wa mazingira na mimi naamini kuwa walio wengi wataendelea kuthamini na kukumbusha jamii juu ya matumizi ya nishati safi huku akiwataka vijana kuwa mabalozi wazuri wa kampeni hii", alisema Ndg Ussi
Katika Wilaya ya Ilemela jumla ya taasisi 61 zinatumia nishati safi ya kupikia kati ya taasisi 256 zilizopo sawa na asilimia 23.8. Hata hivyo, malengo ya Wilaya ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034. Taasisi hizo ni Shule za Msingi na Sekondari za Umma na Binafsi, Vyuo na Hoteli. Pia Wilaya imegawa jumla ya majiko 1725 ya nishati safi ambapo 1700 yaligawiwa kwa mama lishe na majiko 25 yaligawiwa kwa walengwa wa TASAF.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani. Umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.