Watumishi wa Manispaa ya Ilemela wakiwemo walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na watumishi kutoka idara ya afya wamekabidhiwa hati miliki 315 za ardhi ambapo hati 297 zimekabidhiwa kwa walimu na hati 18 zimekabidhiwa kwa watumishi wa idara ya Afya.
Hati hizo zilikabidhiwa na Naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Manispaa hiyo wa kutoa motisha kwa walimu kutokana na juhudi walizofanya katika ufundishaji na kuwawezesha wanafunzi wa Manispaa ya Ilemela kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa kwa darasa la saba, kidato cha nne na sita kwa mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watumishi wake wanapata makazi kwa gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Naibu Waziri wa Ardhi Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kuipongeza halmashauri ya manispaa ya Ilemela kwa uhodari wake katika zoezi la urasimishaji makazi, upimaji na umilikishaji aliwataka watumishi hao kuzitumia hati hizo kwa shughuli za maendeleo.
“Ilemela imekuwa ikifanya vizuri katika mambo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, mtakumbuka hata mwaka jana ilikuwa ya pili kitaifa, Sisi kama serikali tunaona jitihada zenu ndio maana tumetoa utaratibu rahisi wa kuwapatia viwanja kwa walimu wetu ili kuweza kuwapatia motisha katika kazi” Alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya ardhi na mipango miji Ndugu Shukran Kyando alisema kuwa hati hizo zilizotolewa kwa walimu ni sehemu ya viwanja 525 ambavyo vipo kwenye mpango huo wa mradi wa viwanja vya walimu katika eneo la Nyamiswi Kata ya Sangabuye Manispaa ya Ilemela.
Katibu wa kamati ya mradi wa viwanja hivyo, Mwalimu Albert Mahuyu alisema kuwa pamoja na kamati yake kukutana na changamoto mbalimbali wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo, alimshukuru aliyekuwa Mbunge wa Ilemela Mhe. Angelina Mabula kwa kuja na wazo hilo la kutoa motisha ya viwanja kwa walimu pamoja na uongozi mzima wa Manispaa chini ya Mkurugenzi John Wanga kwa namna ambavyo walihakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa.
Nao wanufaika wa mradi huo wa viwanja wamemshukuru aliyekuwa Mbunge wa Ilemela Dkt. Angeline Mabula pamoja na uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa kuwaheshimisha walimu kwa kuweza kupata hati kwa ajili ya kujenga nyumba katika maeneo rasmi hivyo hiyo ni fursa hata wakistafuu kuishi maisha mazuri huku wakishauri Halmashauri nyingine nchini ziweze kuanzisha mradi kama huo ili kuwawezesha walimu na watumishi wengine kuwa na uhakika wa maisha hata watakapo staafu.
Jumla ya Hati 1,596 zilitolewa kwa wananchi mbalimbali wa Manispaa ya Ilemela, wakiwemo walimu na watumishi wa idara ya Afya hii ikiwa ni muendelezo wa ugawaji wa hati na kufanya jumla ya hati zilizotolewa kipindi cha mwaka 2020 kuwa 6,061.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.