Harambee ya uchangiaji wa madawati kwa shule za Msingi Ilemela iliyofanyika takriban miezi minne iliyopita imeendelea kuzaa matunda ambapo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala amepokea jumla ya madawati 50 yaliyogharimu shilingi milioni 4 kutoka kwa benki ya NBC-Mwanza.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya madawati hayo Mhe.Masala amesema lengo la Wilaya ya Ilemela ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anakaa chini sambamba na kuwapatia watoto mazingira bora zaidi ya kujifunza na kujifundishia .
Aidha Mhe.Masala ametoa shukrani kwa benki ya NBC kwa niaba ya timu nzima ya Ilemela kwa kutimiza ahadi yao huku akiwaomba kuendelea kuunga juhudi mbalimbali za maendeleo hususan kuunga mkono zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa linaloendelea kwa shule za msingi za Manispaa ya Ilemela.
“Natambua ushiriki wa benki ya NBC katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo wilayani kwetu,nami nawaahidi kuwa itakapojitokeza fursa ya sisi kufanya kazi na ninyi kupitia huduma mbalimbali za kibenki mnazotoa tutafanya kazi.” Amesema Mhe.Masala.
Meneja wa benki ya NBC-Mwanza ndugu Thomas Lijaji ameeleza kuwa utoaji wa madawati hayo ni moja ya huduma wanazozitoa kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii hususan Wilaya ya Ilemela ambayo pia ni kati ya wateja wake wanaoendelea kupata huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo mikopo ya kuwainua kiuchumi
“Sisi kama NBC tuliahidi madawati 50 na leo tumekuja kuyakabidhi na hatujafunga milango ya kushirikiana na jamii na pale mtakapokuwa na mahitaji yoyote niendelee kuwakaribisha tupo tayari kuendelea kushirikiana nanyi”amesema Ndugu Lijaji
Mhe. Renatus Mulunga Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela akitoa shukurani zake kwa benki ya NBC amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ya madawati ili hata waliochangia waendelee kupata moyo wa kuchangia huku akisisitiza kuendelea kuishi katika kauli mbiu ya Ilemela inayosema “Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga”.
Neema Richard Charles mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kaselya amewashukuru NBC kwa kutoa madawati hayo kwani inaenda kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati huku akiwaomba wasichoke kuendelea kuwasaidia.
Madawati haya 50 yanaenda kupunguza changamoto ya watoto 150 kukosa madawati hili ni jambo kubwa sana kwetu pamoja na hilo tuwaombe tena kutushika mkono katika utatuzi wa changamoto ya vyumba vya madarasa kwa shule za Msingi amesema, Mhandisi Modest Apolinary Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.