Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatarajia kukusanya kiasi cha Tsh 9,024,065,000.00 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga alipokuwa akiwasilisha makisio na mpango wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha 2018/2019 katika Baraza la Waheshimiwa madiwani.
Aidha alisema kuwa kushuka kwa makisio ya mpango na bajeti hiyo kumetokana na kuwa vyanzo vilivyokuwa vikikusanywa na halmashauri kuelekezwa kukusanywa na serikali kuu chini ya usimamizi wa Mamlaka ya mapato (TRA) jambo ambalo limepelekea bajeti ya Halmashauri kupungua kwa asilimia 23 ambayo ni sawa Tshs 2,729,545,000/= ya bajeti.
Aliendelea kwa kusema kuwa endapo vyanzo hivi vingekuwa chini ya Halmashauri bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa upande wa mapato ya ndani makisio yangefikia Tshs 13,119,065,000.00 kwa ongezeko la Tshs 4,095,000,000.00 sawa na asilimia 17 ya bajeti ya sasa.
Sambamba na hilo Mkurugenzi alisema kuwa, ili kuongeza mapato ya ndani, halmashauri imejiwekea mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa mapato yanakusanywa kwa ufanisi kuweza kufikia malengo yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari 3,uboreshaji wa miundombinu ya barabara kupitia wakala wa barabara (TARURA), kuboresha majengo ya kutolea huduma za afya na elimu.Halikadhalika imelenga kuboresha miundombinu ya mialo na masoko,pia kupitia kauli mbiu ya Wilaya “Ilemela ni yetu tushirikiane kuijenga”, wannachi wataendelea kuhamasishwa juu ya uchangiaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wahisani na wadau wa maendeleo.
Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Wilbard Kilenzi kwa niaba ya Mstahiki Meya aliwashukuru watendaji kwa maandalizi mazuri ya mpango na bajeti na kuwataka kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kujituma ili kutekeleza yale yote yaliyopangwa ili kuweza kufikia malengo ambayo yamewekwa.
Jumla ya kiasi cha Tsh. 68,613,400,00.00 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 zilipitishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jana tarehe 27/02/2018 ambapo kati ya fedha hizo Tshs. 15,013,332,000.00 ni fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo, Tshs 1,620,686,000.00 ni fedha za ruzuku ya matumizi ya kawaida, Tshs. 42,75,317,000.00 ni kwa ajili ya mishahara, na Tshs. 9,024,065,000.00 ni fedha ya mapato ya ndani.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.