Shirika lisilo la kiserikali la WADADA linaloshughulika na masuala ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,ulinzi na utetezi wa haki za watoto na mabinti limetambulisha mradi wake mpya unaotambulika kwa jina la “HAKI YA BINTI”kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Mradi huu unatarajia kufanya kazi ndani ya Manispaa ya Ilemela ukihusisha kata mbili Kitangiri na Pasiansi ambapo wadau na wataalam mbalimbali wa afya, elimu ,vyombo vya ulinzi na usalama watahusishwa.
Akiutambulisha mradi huo mpya, Mwenyekiti wa bodi, Ndugu Amri Linus alisema kuwa, anategemea kuwa jamii nufaika inapata mabadiliko makubwa kwa kuangalia namna wanavyoweza kujikinga na ukatili wa kijinsia pamoja na kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa wa nini maana ya haki ya binti.
Bi.Anitha Samson ambae ni mratibu mradi amesema mradi utahusisha mabinti kuanzia umri miaka 7 mpaka 25 ambapo lengo kuu la mradi ni kuwajengea uwezo mabinti katika kupambana na matukio ya ukatili na unyanyasaji ndani ya jamii.
“Tunatamani mabinti wote wawe na uwezo wa kutambua na kupaza sauti zao pindi wanapoona viashiria au wanapofanyiwa ukatili wa aina yoyote ile,lakini pia wawe msaada kwa wengine wasioweza kuzungumza kwa kuwaelewesha na kuwasemea.”amesema
Sambamba na hilo Bi.Anitha amesisitiza kuwa wamejipanga katika kuwawezesha mabinti kiuchumi ,kutoa elimu ya stadi za maisha na elimu ya ujasiliamali kulingana na mzingira waliopo,ili waweze kujisimamia na kuendesha maisha kwa kujiamini na kuepuka vishawishi.
Nae Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii ndugu Sitta Singibala amelishukuru shirika la WADADA kwa ujio wa mradi huo ndani ya Ilemela.
“Natambua kuwa nyie ni wadau wetu kwa muda mrefu sasa na kazi zenu nyingi zinaendelea kuleta matokeo mazuri maeneo mlikopita kwani kumekuwa na ongezeko la uelewa kwa jamii juu ya mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.Tunajivunia shule ya sekondari Mihama kwa uthubutu wao katika kuhamasisha jamii juu ya kutonyamazia matukio ya ukatili”
Aidha Mkurugenzi wa shirika la WADADA Bi.Ruth John ameitaka jamii ya Ilemela hashasa mabinti kujitambua na kuwa huru kuwaona punde wanapoona matukio ya ukatili.
“Mabinti zetu wa Ilemela tunawapenda sana ,tupo kwa ajili yenu msisite kutufikia kwa ushauri au msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji.”alisema
Akihitimisha zoezi hilo la utambulisho wa mradi, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ndugu Godfrey Mzanva ambae ni Afisa Tarafa wa Ilemela amesema
“Ni wajibu wetu kuwatambua, kuwafikia na kuwalinda mabinti wote.Kusiwe na “gap”kati ya walimu na watoto mashuleni.Walimu na wazazi watambue kuwa wanapaswa kuwa marafiki wa watoto na wawalee katika mazingira rafiki ya kumfanya mtoto kuwa huru kutoa changamoto zake. Jamii ya Ilemela tusinyamaze pindi tunapoona matukio ya ukatili wa kingono na ukatili wa aina yoyote ile ndani ya jamii yetu.Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo tayari kutoa ushirikiano na kutokomeza kabisa ukatili ”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.