"Malengo ya serikali ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan ni kwamba kufikia mwaka 2032 wananchi wote wawe wameondokana na nishati zinazodhuru na kupata nishati safi kwa afya zao."
Kauli hiyo imetolewa na Mhe.Dkt.Angeline Mabula(Mb) wa Ilemela alipokuwa akizungumza na kina mama wajasiriamali wa Ilemela katika hafla ya kuwakabidhi gesi kina mama hao.
Mhe.Mabula amesema kuwa ni ajenda ya serikali ya awamu ya sita kumpunguzia mama mahangaiko ya muda mrefu na kumpatia nishati mbadala ya gesi ili kukamilisha kazi zake za upishi haraka na kupata muda wa kufanya shughuli za kujiingizia kipato zaidi kiuchumi.
" Naamini wote tunakubaliana kwamba gesi ni nishati mbadala rafiki wa mazingira, naomba tuwe makini katika matumizi yake ili tusilete athari mbaya katika mazingira yetu."
Sambamba na hayo Mhe.Dkt Mabula ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo katika sekta mbalimbali za afya, elimu n.k.
Tunawashukuru REA kutoka wizara ya nishati kwa kuunga mkono juhudi za Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya utunzaji wa mazingira nchini kwa kutoa mitungi hii ya gesi." Amesema Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala aliekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
" Tutaendeleakuunga juhudi za Rais wetu kwani hajatuangusha.Anafanya kazi nzuri inayoonekana ."
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amewaasa wana Ilemela kuendelea kuyaishi mazuri yote yanayofanywa na viongozi wetu kwa kuwa tunaona maendeleo yanavyokuja kwa kasi ndani ya Manispaa ya Ilemela.
Aidha elimu ya juu ya utunzaji wa mazingira imetolewa kutoka kwa mtaalam wa wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ndugu William.
" Ni muhimu kutunza mazingira kwani ndio sehemu tunayoishi.Faida za miti ni nyingi kwetu ikiwa ni pamoja na kupata matunda, vivuli na hewa safi ya oksijeni ambayo ni hewa muhimu kwa binadamu." Amesema William
Anna Masalu ni mama lishe kutoka kata ya Nyamhongolo yeye anamshukuru Mhe.Mabula kwa kutoa gesi hizo.
" Namshukuru Mama Mabula kwa hii zawadi itanisaidia sana katika shughuli zangu za mapishi, yaani sasa hivi mteja akija kila kitu fasta tu."
Jumla ya mitungi 400 ya gesi imetolewa na wizara ya nishati kupitia REA katika kuunga mkono jitihada za mbunge wa Ilemela Mhe.Mabula na kukabidhiwa kwa kina mama wajasiriamali wa Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.