Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Mhandisi Modest Apolinary amewataka watendaji katika kata ya Nyamanoro kuhakikisha wanatumia fedha za ujenzi wa madarasa mapya kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata ya Nyamanoro huku akiwataka wananchi wa kata hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo uboreshaji wa sekta ya elimu.
'.. Tumeshawawekea kwenye akaunti yenu milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya mawili, Mkatumie fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ..' Alisisitiza
Aliendelea kufafanunua kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi milioni arobaini zimetolewa na Serikali Kuu kupitia mpango wa matokeo kutokana na ufanisi (EP4R) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Mkudi kata ya Nyamanoro ili kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
Pamoja na hayo, Mhandisi Modest amesema kuwa kupitia mapato ya ndani shule za msingi Mkudi na Mji Mwema zimetengewa kiasi cha shilingi milioni saba na laki tano kila moja kwa ajili ya ukamilishaji wa madarasa yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ikiwa ni mchango wa halmashauri katika kuunga mkono nguvu za wananchi wake.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Nyamanoro Mhe Maganiko Ngaka mbali na kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ya elimu katika kata yake amempongeza mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela kwa kufika katika kata yake na kutembelea maeneo ya kata yake kusikiliza kero na changamoto zinazowakabiki wananchi wake huku akiahidi kuendelea kushirikiana nae katika kuwaleta maendeleo wananchi wa kata hiyo
Nae Mkuu wa shule ya msingi Mkudi Bi Zuhura Ally Bilal amemshukuru mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela kwa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa mapya na kumalizia yale ya awali kwani kitendo hicho kitasaidia kupunguza changamoto iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu ya upungufu wa vyumba vya madarasa
Katika ziara hiyo Mhandisi Modest alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa kata hiyo pamoja na kukagua miradi ya barabara, elimu na masoko.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.