Jumla ya vikundi 37 vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya manispaa ya Ilemela inayojumuisha asilimia 4 kwa ajili ya wanawake,asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu vimepatiwa mafunzo sambamba na zoezi la ujazaji wa mikataba ya mikopo ambayo inatarajiwa kutolewa katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza wakati wa zoezi la kujaza mikataba na utiaji saini wa mikataba ya ukopeshaji fedha kwa vikundi hivyo lililofanyika katika ukumbi wa manispaa ya Ilemela Afisa maendeleo wa manispaa ya Ilemela Bi Amina Bululu amewataka wana vikundi hao kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa ajili ya miradi iliyokusudiwa sanjari na kuhakikisha wanarejesha fedha hizo katika muda uliopangwa kulingana na mkataba bila riba yeyote.
“ Ni utaratibu wetu wa kawaida kutoa mafunzo haya ya kukumbushana matumizi bora ya fedha mnazokopeshwa hasa tunapokutana kwa pamoja kama hivi ili zilete tija katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mnazofanya na kufanya zoezi la kukopesha liwe endelevu.”
Aidha Bi. Bululu amevipongeza vikundi vya wanawake kwa marejesho mazuri ya fedha hizo za mkopo huku akiviasa vikundi vya vijana na watu wenye ulemavu kuhakikisha navyo vinarejesha kwa wakati ili viweze kupata fedha nyingi zaidi na kukuza biashara sambamba na kuongeza kipato chao.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya vijana manispaa ya Ilemela Bi Lucy Nicholaus Matemba amevitaka vikundi vinavyokopeshwa na manispaa kuhakikisha vinayaishi makubaliano yaliyo katika mkataba pamoja na kusisitiza kuwa wasiache kuwatumia maafisa maendeleo walio katika maeneo yao au wale wa makao makuu ya wilaya pindi zinapojitokeza changamoto zozote.
Monika Makaranga ni mwenyekiti wa kikundi cha Tupendane group 2020 kilichopo Msumbiji kata ya Kawekamo kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku ,usindikaji wa vyakula ambavyo ni viungo na unga wa lishe,kwa niaba ya kikundi chake ameishukuru Manispaa ya Ilemela kwa kukubali kuwapatia mkopo awamu nyingine wa shilingi milioni 10 ambayo wanatarajia kuitumia kwa mradi mpya wa bajaji.
Nae Bi. Judith Kasuja Joseph ambae ni mlemavu wa miguu kutoka kata ya Kahama mtaa wa Isela ameipongeza manispaa hiyo kwa uwepo wa masharti mepesi upande wa walemavu katika kupata mkopo.
Halmashauri ilitenga jumla ya kiasi cha shilingi milioni 285,000,000 inayotarajiwa kutolewa kwa vikundi 37 ndani ya manispaa ya Ilemela kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.