Elimu ya Lishe sambamba na njia bora za unyonyeshaji imeendelea kutolewa kwa jamii ya Ilemela hususan wakina mama wanaonyesha na wanaotarajiwa kujifungua.
Wakina mama hao wametakiwa kujali lishe bora kwa familia zao hasahasa kwa kina mama wanaonyesha na watoto ambao wapo katika hatua za ukuaji kwa kuzingatia kuwa uimara na ubora wa akili ya mtu mzima huanza kutengenezwa kwa viwango pindi mtu anapokuwa mdogo kwa kupitia lishe anayopata kwa wakati huo.
Akitoa elimu hiyo ya lishe na namna ya unyonyeshaji bora kwa wakina mama waliohudhuria kliniki zao za kawaida katika kituo cha afya Buzuruga, Muuguzi Bi Asteria Athanas amewakumbusha kuwa, lishe bora ni kula mlo kamili na wa kutosha wenye mchanganyiko wa viini lishe vyote vinavyotakiwa mwilini kutoka makundi matano ya vyakula ambayo ni wanga, protini, sukari na mafuta pamoja na vitamin na madini.
Wakinamama hao wamepata fursa ya kufahamu mambo mbalimbali kuhusu lishe ikiwa ni pamoja na faida za unyonyeshaji kwa watoto wachanga maziwa ya mama pekee kuanzia umri wa 0 hadi miezi 6, ambapo huboresha ukuaji, uimarisha kinga ya mwili kwa mtoto na kuboresha mahusiano baina ya mama na mtoto.
Bi Asteria akizitaja faida za unyonyeshaji mzuri amesema kuwa ni pamoja na kupunguza uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi au kiriba tumbo kwa mtoto na kumfanya kuwa na akili nzuri huku akisisitiza kuwa jukumu la kupata lishe bora kwa familia sio la mama peke ake bali ni la wanafamilia wote.
Nae Damaris Dawson ambae ni muuguzi wa kituoni hapo amewataka kina mama kuwaongezea lishe zaidi watoto baada ya miezi sita kwani itamfanya mtoto akue vizuri na kumrahisishia mama kuendelea na majukumu yake mengine ya uzalishaji kiuchumi.
Judith Mgeta na Pili Kilanda ni wakina mama waliofika katika kituo hicho cha Afya cha Buzuruga wamewashukuru wataalam kwa kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya afya hususan elimu hiyo ya lishe bora na njia bora za unyonyeshaji huku wakiomba elimu hiyo iendelee kuwafikia wengi zaidi
“Tunaishukuru sana serikali yetu hususan Manispaa yetu ya Ilemela kwa kuweka utaratibu huu wa sisi kina mama kupata elimu mbalimbali kama hizi hatujasoma lakini tunaweza kupata uelewa wa vitu vingi vya afya kupitia mikusanyiko kama hii ,tunaomba utaratibu huu uendelee na kuwafikia wakinamama wengi zaidi, kwani ni msaada mkubwa mno kwetu” Wamesema
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.