Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini wameendelea kupatiwa elimu ya fedha itakayowawezesha kuongeza ufanisi katika shughuli za kuongeza kipato, uwekezaji sahihi pamoja na uwekaji wa akiba.
Elimu hiyo imetolewa tarehe 03 Julai, 2025 na afisa maendeleo wa kata ya Ilemela, Bi. Kundi Anthony wakati wa zoezi la malipo dirisha la mwezi Machi hadi Aprili 2025 linaloendelea katika mitaa yote 171 ya Manispaa ya Ilemela.
Bi. Kundi alifafanua kuwa bila uelewa mzuri wa jinsi fedha zinavyofanya kazi, inaweza kuwa vigumu kufikia mafanikio ya kifedha na hatimaye kushindwa kujikwamua kiuchumi kama kusudio la mpango linavyoelekeza.
Nae Ndugu Leonard Nyamgenda, mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela amewasisitiza wanufaika kuendelea kubaki kwenye vikundi vya ujasiriamali na wale ambao hawajajiunga kwenye vikundi waweze kufanya hivyo ili kuwawezesha kuongeza kipato na kukopeshana wenyewe kwa wenyewe kwa masharti nafuu.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa TASAF Bi. Anjela Lugendo mkazi wa mtaa wa Butuja ameishukuru serikali kwa kuwawezesha kiuchumi, kwani kupitia fedha hizo ameweza kuongeza mtaji wa biashara yake ya kuchoma mahindi ambapo kwa ushirikiano na mwenza wake amefanikiwa kujenga nyumba ya kuishi na kusomesha watoto
"Ninaishukuru serikali kupitia TASAF nimeweza kujenga nyumba pamoja na kusomesha watoto wangu, nimenufaika na mradi huu kwa kushirikiana na mme wangu tunakaribia kuhamia kwenye nyumba yetu, nimeongeza mtaji wangu wa kuchoma Mahindi,nashukuru nimeweza kufikia malengo yangu kwa uchache wake", amesema bi Anjela
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.