Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewapongeza wananchi wa mtaa wa Zenze kata ya Kiseke kwa kuchangia na kuanza ujenzi wa barabara ya Km 2 inayotoka maungio ya barabara ya Lami ya Sabasaba Kiseke hadi Nyasaka kwa kiwango cha changarawe
Pongezi hizo amezitoa wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa kata ya Kiseke na Ilemela kwaajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi ndani ya jimbo hilo ambapo amesema kuwa wananchi wa mtaa wa Zenze wametekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya jimbo la Ilemela ya kwamba ‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’ baada ya hao wenyewe kuona kero inayowasumbua na kuanza kujichanga kwaajili ya utatuzi
‘.. Utekelezaji wa mradi huu umesadiki kauli mbiu yetu ya wilaya, Wananchi mmeona kero mkaanza wenyewe kuitatua badala ya kusubiria Serikali, Nawapongeza sana hii ni kazi kubwa mlioifanya ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula ameahidi kuchangia mifuko mia moja kwa wananchi hao kama ishara ya kuunga mkono juhudi walizozifanya kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo pamoja na kumshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya jimbo lake ikiwemo ya maji, afya, barabara na elimu
Kwa upande wake mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga amefafanua kuwa ili kuunga mkono kilichofanywa na wananchi hao atawasiliana na wakala wa barabara za mijini na vijijini TARULA kuhakikisha wananchi hao wanapata msaada wa kitaalamu kwaajili ya ujenzi wa barabara hiyo sanjari na manispaa yake kuona namna nyengine borra zaidi ya kusaidia changamoto zinazokabili ukamilishaji wa ujenzi huo
Nae Diwani wa kata ya Kiseke Mhe Mwevi Ramadhan mbali na kuipongeza kamati ya ujenzi kwa kuratibu zoezi hilo la ujenzi, amesema kuwa manispaa ya Ilemela ipo kwenye mpango wa kununua mitambo mipya kwaajili ya ujenzi wa barabara za mitaa hivyo kukamilika kwa mpango huo kutasaidia ukarabati wa barabara za mitaa kwa gharama nafuu na ufanisi
Frank Geofrey ni mwananchi wa mtaa wa Zenze, Yeye ametaja changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ikiwemo ukosefu wa usafiri wa uhakika hasa katika vipindi vya mvua, vifo kwa wajawazito vinavyotokana na kutofika kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapohitaji kujifungua pamoja na wanafunzi kushindwa kufika shuleni nyakati za mvua
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.