DIWANI WA KATA KAWEKAMO AIPONGEZA SHULE SEKONDARI KILIMANI
Diwani wa kata ya Kawekamo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mheshimiwa Japhesi Rwehumbiza amefanya hafla fupi ya kuipongeza shule ya sekondari Kilimani kwa jitihada walizozionyesha katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kwa mwaka 2016 lengo ikiwa ni kuwapa motisha walimu wa shule hiyo.
Hatua hiyo ya kuipongeza shule hiyo imefikiwa baada ya walimu kuonyesha jitihada katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2016 kwa kuliganisha na matokeo ya 2015 ambapo shule hiyo ilishika nafasi ya mwisho kiwilaya
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mheshimiwa Japhesi mbali na pongezi hizo amewataka walimu wa shule hiyo kupendana, kushirikiana na kuzingatia maadili ya kazi yao pamoja na kukemea suala la mimba kwa wanafunzi mashuleni ili kuyafikia malengo ya Serikali kwa kutoa elimu bora itakayosaidia kufikiwa kwa Tanzania ya Viwanda
“Hatuwezi kuifikia Tanzania ya Viwanda bila kuzalisha wataalamu , sasa kama tutashindwa kupenda, kushirikiana na tukakubali kuvunjwa kwa maadili kwa kuruhusu wanafunzi wapate mimba tutakuwa hatulitendei haki Taifa hili, nia yangu ni kuona walimu wangu hampati tabu yeyote na kama kuna mwalimu wangu ambae bado hajapata nyumba anijulishe ili niweze kutatua changamoto hiyo, nitazidi kuwapongeza kwa kila mtakapokuwa mnafanya vizuri ili tuyafikie malengo kwa pamoja”, Alisisitiza.
Pamoja na hayo, Mhe Japhes alichangia pesa kiasi cha Shilingi laki na moja nusu kwa ajili ya kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo utengenezaji wa madirisha jambo ambalo liliungwa mkono na Mhe Innocent Mwinyikondo wa kata ya Kiseke ambae alihudhuria hafla hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kilimani Mwalimu Kicheta Kicheta kwa niaba ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo mbali na kumshukuru Diwani wao kwa kuwa pamoja nao na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wamemuhakikishia kuwa wataongeza jitihada kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.