Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kwa jina la machinga wametakiwa kuwapuuza wanasiasa wanaowashawishi kutoka katika maeneo rasmi yaliyotengwa na Serikali kwaajili ya kufanyia biashara zao.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati akizungumza na wafanya biashara wa masoko ya Kabwaro, Buzuruga, Nyasaka na Kiloleli wakati wa ziara yake ya kutembelea masoko hayo kwaajili ya kusikiliza kero, changamoto na maoni ya wafanyabiashara juu ya utekelezaji wa shughuli za kila siku tangu kutengwa kwa maeneo rasmi ya biashara baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan la kutenga maeneo rasmi na rafiki kwaajili ya shughuli za kibiashara ambapo amewataka wafanya biashara wadogo kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili, kuweka mazingira rafiki ya biashara ili kujikwamua kiuchumi badala ya kurudi katika maeneo hatarishi yasiyofaa kwa shughuli za biashara jambo linalorudisha maendeleo nyuma.
‘.. Wapo watu wasiowatakia mema wanapita kuwashawishi mrejee katika maeneo hatarishi tuliowatoa hapo awali, Msikubali Serikali yenu ni sikivu itaendelea kushirikiana nanyi kutatua kero zote zinazowakabili mkiwa hapa hapa sokoni, atakaetoka nje ya soko lililotengwa na Serikali kitakachompata shauri yake ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala amewahakikishia wafanya biashara hao kuwa Serikali itaendelea kuboresha maeneo yao ya kibiashara ikiwemo kuweka miundombinu ya barabara, umeme, maji, vyoo na kudhibiti vitendo vya kiharifu ili waweze kufanya biashara kwa amani na utulivu huku akiwataka kuendelea kuiunga mkono Serikali yao katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amefafanua kuwa manispaa yake imetenga fedha kwaajili ya ukarabati wa miundombinu ya masoko na itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanya biashara hao huku akiahidi kutengeneza barabara ya soko la Nyasaka hivi karibuni ili iweze kufikika kwa urahisi.
Abdulrahman Simba ni diwani wa kata ya Nyasaka amemshukuru mkuu wa wilaya ya Ilemela kwa kutembelea masoko ya kata yake huku akiwaasa wananchi wa kata yake kuhakikisha hawatoki nje ya maeneo rasmi yaliyotengwa na Serikali kwa shughuli za biashara ndogo ndogo.
Akihitimisha Bwana Samuel Mwita mfanyabiashara kutoka soko la Nyanda Nyasaka kwa niaba ya wafanyabiashara wengine wa soko hilo amelalamikia wizi kwa njia ya kishirikina unaofanyika katika soko hilo baina ya wafanyabiashara maarufu kama ‘chuma ulete’ huku akitaka viongozi kutafuta ufumbuzi juu ya kero hiyo inayowasababishia hasara na kufilisika mitaji yao .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.