Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hassan Masala ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Jijini Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha inaweka utaratibu rafiki kwa wananchi katika kusambaza maji ili kuondoa usumbufu usio wa lazima
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi wa kata ya Mecco na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata hiyo.
Mhe Masala amesema kuwa ni wajibu wa MWAUWASA kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri wa kusambaza maji kutokana na kwamba Serikali ya awamu ya sita inafanya jitihada kubwa katika kuondoa kero hii ya maji ambayo imekuwa ya muda mrefu sasa..
Akifafanua kuhusu kero ya maji amesema kuwa kwa wilaya ya Ilemela pekee imeshapokea magari ya kutosha ya mabomba ya kusambazia maji katika maeneo ambayo yanakabiliwa na upungufu wa maji kwa kiasi kikubwa
Ameongeza kusema kuwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyanzo vipya vya maji vya Butimba na matarajio ya kuanzisha chanzo kipya cha Kabangaja ili kusaidia upataikanaji wa maji ya uhakika kwa wananchi wa Ilemela na mkoa wa Mwanza kwa ujumla wake
Kwa upande wake meneja msaidizi wa idara ya maji MWAUWASA Kanda ya Nyakato Ndugu Juma Saidi mbali na kukiri kupokea fedha nyingi kutoka Serikali kuu kwaajili ya kuboresha sekta ya maji amesema kuwa mamlaka hiyo inaendelea na taratibu za kusambaza maji kwa wananchi kulingana na utaratibu uliowekwa ili kuhakikisha kila eneo lenye changamoto linapatiwa ufumbuzi pamoja na kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati mamlaka hiyo ikiendelea na kazi zake
Nae diwani wa kata ya Mecco Mhe Godlisten Kisanga amemshukuru mkuu huyo wa wilaya ya Ilemela kwa jitihada zake katika kutatua kero za wananchi sanjari na kuwaomba wananchi kuungana na Serikali katika kufanikisha shughuli za kila siku za maendeleo
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Masala amehitimisha ziara yake kwa kuwaahidi wananchi wa kata ya Mecco kurudi katika eneo la shule ya Kilimanjaro hapo kesho kwaajili ya utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliowasumbua kwa muda mrefu ili kuupatia ufumbuzi
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.