Mhe Hasan Masala mkuu wa wilaya ya Ilemela amepiga marufuku michango kwa wanafunzi na wazazi katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo ndani ya wilaya hiyo.
Katazo hilo limekuja mara baada ya malalamiko yalitolewa na wazazi mbalimbali juu ya michango shuleni wakati ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata ya Buzuruga, ambapo amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwaajili ya kugharamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za elimu na kuboresha miundombinu ya sekta hiyo ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo, madawati hivyo kutokuwepo kwa ulazima wa kuchangisha wananchi ili watoto waweze kupata elimu
Aidha aliongeza kusema kuwa iwapo kuwa kama kutakuwa na ulazima wa kuchangia kwa makubaliano ya wazazi na uongozi wa shule basi lazima ofisi yake iweze kutoa kibali na kushirikishwa juu ya uwepo wa michango hiyo
‘… Upo muongozo wa utoaji elimu bila malipo kwa maana ya bure sio utashi wangu, Wajibu wetu ni kusimamia maelekezo ya serikali juu ya usimamizi wa elimu, Tunatambua uwezo wa wazazi unatofautiana kuna watu wanaiona elfu moja ni kidogo lakini kuna watu wanatafuta elfu moja ndani ya wiki na hawaipati …’ Alisema
Daniel Lushinge ni mwananchi wa kata ya Buzuruga aliyelalamikia uwepo wa usumbufu wakati watoto wanapofata huduma ya elimu katika shule ya msingi Buzuruga pamoja na adhabu kwa watoto wasiochangia fedha kwa ajili ya masomo ya ziada ambapo ameiomba serikali kufuatilia kwa umakini juu ya walimu wasio waadirifu wanaochangisha wazazi nje ya utaratibu wa serikali
Kwa upande wake Afisa elimu sekondari wa Manispaa ya Ilemela Mwalimu Sylvester Mrimi amekemea vikali walimu wote watakaojihusisha na zoezi la kuchangisha wazazi mashuleni na kusisitiza kuwa hairuhusiwi kuchangisha wala kumzuia mwanafunzi kupata masomo kwa kigezo cha michango na kwamba mwalimu yeyote atakejihusisha na kukusanya michango shuleni atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga amempongeza kumpongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutatua kero za wananchi huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha za maendeleo na mbunge wa jimbo hilo Dkt Angeline Mabula kwa ushirikiano anaoutoa katika shughuli za maendeleo
Mhe Masala amehitimisha kwa kuwasisitiza walimu kuzingatia taratibu za utoaji wa adhabu mashuleni sanjari na kuwataka wazazi kutowalea watoto nje ya maadili na kuwafanya kuwa wavivu na wajinga.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.