Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Masala amesitisha ujenzi kwa wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo la shule ya sekondari Busenga inayoendelea kujengwa katika mtaa wa Busenga.
Akizungumza na wananchi wa kata za Buswelu na Nyamhongolo wanaoishi jirani na eneo inapojengwa shule ya sekondari Busenga Mhe Masala amewataka wananchi wanaoishi eneo hilo kuacha mara moja shughuli zote za ujenzi wa nyumba za kuishi na maendelezo mengine Ili kutoa fursa kwa timu ya wataalam aliyoiunda kutoka vyombo vya usalama na maafisa ardhi kujiridhisha juu ya uhalali wa umiliki wa eneo hilo
'.. Iwe umepewa eneo na mkurugenzi, Iwe umepewa na afisa mipango miji, Iwe una nyaraka, Iwe una kibali na umepewa na mtu yeyote kutoka mamlaka yeyote naomba ujenzi usifanyike ..' alisema
Aidha Mhe Masala amewataka wananchi wa eneo hilo kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia mbili kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 110 kwenye shule 23 za manispaa pamoja na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Kwa kuwa kiunganishi katika Utekelezaji wa shughuli za maendeleo
Kwa upande wake Afisa elimu sekondari wa Manispaa ya Ilemela Mwl Sylvester Mrimi amefafanua kuwa upo uhitaji mkubwa wa kujengwa shule ya sekondari Busenga Kwani shule za Bujingwa na Buswelu zimejaa wanafunzi wengi kuliko uwezo wake na kwamba watoto wengi wanatoka mtaa wa Busenga
Nae Bwana Benedict Amoro mpima kutoka idara ya Ardhi na mipango miji manispaa ya Ilemela akasema kuwa eneo hilo ni salama Kwa matumizi ya taasisi za shule, Limepimwa na kupangiwa matumizi ya ujenzi wa shule ya msingi upande wa chini na ujenzi wa shule ya sekondari Kwa upande wa juu
Diwani wa kata ya Nyamhongolo Mhe Andrea Nginila na diwani wa Buswelu Mhe Sara Ng'wani mbali na kumshukuru Rais Mhe Samia wameahidi kusimamia fedha zote za maendeleo zitakazotolewa katika maeneo Yao huku mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela akisistiza umuhimu wa kuwekeza katika Elimu Kwa vizazi vijavyo
Ziara ya mkuu wa wilaya ya Ilemela imejumuisha wataalam wa idara na vitengo vya manispaa ya Ilemela, wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine ikiwemo TANESCO na MWAUWASA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.