“Kama unaona elimu ni gharama basi jaribu ujinga”, ni maneno ambayo ameyanukuu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hasan Masala wakati akikabidhi madawati kwa shule za msingi za Ilemela.
“Sisi tumeona tusijaribu ujinga lazima tuwekeze katika elimu ambayo imegawanyika katika makundi mbalimbali kuanzia elimu ya awali hadi ya chuo kikuu na ili kuwa na Taifa lenye watu wenye kuelewa wajibu wao ni lazima tuwekeze kwao angali wachanga”, amesisitiza
Mhe Masala ameongeza kwa kusema kuwa Ushirikiano ndio nguzo pekee katika kufanikisha kila jambo ambalo tunapanga kufanya kwa pamoja, jamii nzima ya Ilemela tunalo jukumu la kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita kwa kushiriki kwa namna mbalimbali katika shughuli za kujiletea maendeleo.
Pamoja na hayo amewashukuru wadau mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki katika kufanikisha upatikanaji wa madawati hayo 1500
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Halmashauri na wadau wote walioshiriki kutufikisha hapa tulipo leo kwa kujitoa kwenu kupatikana kwa kiasi hiki cha madawati, lengo letu lilikuwa ni kupata madawati 1000 kwa awamu ya kwanza lakini tumevuka lengo kwa asilimia 50 hii yote ni katika kumuunga mkono Rais wetu Mhe.Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya elimu.Tujivunie watoto wetu wanapokuwa katika mazingira mazuri ya kupata elimu kwani hata ufaulu utaongezeka.” Amesema Masala.
Ameongeza kwa kusema kuwa jitihada hizi za maboresho katika sekta ya elimu zinaendelea katika ngazi ya Wilaya na mkoa ambapo amebainisha kuwa tayari mkoa wa Mwanza umeanza oparesheni kabambe ya kuondoa upungufu wa madarasa lengo ikiwa ni kupunguza na kuondoa kabisa changamoto ya uchache wa vyumba vya madarasa ndani ya mkoa mzima wa mwanza.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga ameshukuru wananchi na wadau wote waliofanikisha upatikanaji wa madawati hayo kama moja ya njia ya kurahisha ukaaji mzuri wa mpangilio.
“Taifa lolote duniani likipata elimu hakika maendeleo yanapatikana,yote haya yamewezekana kwa sababu ya ushirikiano mkubwa wa uongozi wa Ilemela na wadau mbalimbali wa maendeleo,hatutochoka kusema tunashukuru sana na ninaomba ushirikiano huu uendelee katika kuijenga Ilemela yetu.” Amesema Mhe.Mulunga
Daniel Andrew, na Juliana Anthony ni wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Buswelu ambayo ni moja ya shule iliyonufaika na ujio wa madawati hayo 1500 wametoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wote wa Ilemela kwa wote waliofanikisha upatikanaji wa madawati haya kwani utaenda kuondoa adha ya wanafunzi hao kukaa chini hivyo kuongeza ufaulu katika masomo yao, huku wakitoa ahadi ya kusoma kwa bidii ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Sisi wanafunzi wa Ilemela tunatoa shukrani zetu za dhati kwa uongozi wa juu wa serikali kuanzia kwa Mhe.Samia Suluhu Hassan na ngazi zote za chini,tunaahidi kusoma kwa bidii na kuzidi kuthamini juhudi hizi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali wa elimu.
Niendelee kuisisitiza jamii na kuwaomba kuendelea kuunga mkono jitihada hizi za kuchangia miundo mbinu kama madawati na vyumba vya madarasa zaidi katika kuhakikisha watoto wanasoma na kukaa katika mazingira rafiki amesema Bi Jamila Khalfan ambae ni Kaimu Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilemela
Upatikanaji wa madawati haya 1500 kwa shule za msingi 17 ni matokeo ya harambee iliyofanyika tarehe 31/05/2022 iliyokuwa na lengo la kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za msingi za Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.