Mhe Hassan Elias Masala ameitaka jamii ya Sangabuye kuhakikisha inashiriki kwa kuchangia nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa zahanati ya Sangabuye unaoendelea na kusisitiza kuzingatia ubora na ufanisi wa ujenzi wa zahanati hiyo.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea katika kata hiyo ambapo alipata fursa ya kukagua ujenzi wa zahanati mpya inayojengwa katika kata ya Sangabuye kupitia fedha za mradi wa kunusuru kaya maskini TASAF.
Aidha Mhe Masala amekemea ubadhirifu wa vifaa vya ujenzi vitakavyoletwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakaeiba au kuhujumu kwa namna yeyote ile utekelezaji wa mradi huo uweze kufika tamati
‘.. Hatutaki mgogoro katika utekelezaji wa mradi huu, wananchi tunaowajibu wa kuhakikisha tunashiriki kwa asilimia mia, kwa kufuata miongozo na taratibu za utekelezaji wa mradi huu, Fedha ikipotea hapa hakuna maneno mimi natia pingu’ Alisema
Nae mratibu wa mradi wa kunusuru kaya masikini TASAF wilaya ya Ilemela Leonard Robert amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu kutoka sasa na kwamba changamoto kubwa iliyokuwa ikiukabili ambayo kwa sasa imeshatatuliwa ni kuchelewa kufunguka kwa mifumo ya malipo ya benki kuu hivyo kushindwa kufanya malipo
Gabriel Remmy ni mhandisi wa manispaa anaesimamia mradi huo ambapo amesema kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 15 kwa jengo la wagonjwa wa nje na asilimia 10 kwa jengo la nyumba ya mtumishi huku akiahidi kuusimamia mradi huo kwa ufanisi na umakini ili lengo lililokusudiwa liweze kutimia
Mhe Renatus Mulunga Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni diwani wa kata ya Sangabuye mbali na kumshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuitembelea kata yake amefafanua kuwa kero kubwa inayoikabili kata yake kwa sasa ni changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama, upatikanaji wa umeme na mtandao hivyo kuomba kushirikiana na mkuu huyo wa wilaya kwaajili ya kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.
Ujenzi wa zahanati hiyo ya Sangabuye unatarajia kutumia kiasi cha shilingi Milioni 149 hadi kukamilika ambapo majengo yanayojengwa ni pamoja na jengo la wagonjwa wan je (OPD), jengo la kitengo cha chanjo (RCH) na nyumba ya mtumishi .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.