Mhe Hassan Masala Mkuu wa wilaya ya Ilemela amefanya ziara ya kikazi iliyokuwa na lengo la kukagua hali ya mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza sambamba na ukaguzi wa mialo ikiwa ni pamoja na kufikisha taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu katika kata za Kayenze, sangabuye, bugogwa
Akikagua maendeleo ya mwenendo wa kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali, Mhe Masala, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanaripoti shule sambamba na kuwalinda watoto hao dhidi ya matendo ya kikatili huku akipiga marufuku ya watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi hususan muda wa masomo.
“Watoto ni wa kwetu sote na jukumu la kuwasomesha na kuwalinda ni letu sote kwani watoto ni mali ya jamii” amesema
Aidha amewataka wanafunzi kuwafikishia ujumbe wanafunzi wenzao ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na hawajaripoti shule kuhakikisha wanaripoti shule kwani masomo yameshaanza na hakutakuwa na marudio.
“Waambieni waje shule, kwa ambao hawajakamilisha mahitaji ya shule kama vile sare, madaftari wafike shule wakiwa na sare za shule za msingi hadi watakapopata lengo ni kuhakikisha wote mnasoma kwa pamoja na pia nasisitiza kuwa hakuna mchango wowote ambao utamuondoa mwanafunzi shule”
Pamoja na hayo Mhe Masala amewahimiza wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma na kuacha kukimbilia mambo mengine huku akiwataka kuwa mabalozi wa kusemea umuhimu wa elimu
“Wanafunzi msome, mjali sana elimu kwa sababu ndicho kimewaweka hapa elimu ni kila kitu, tumezungukwa na jamii ambayo bado inatakiwa kujua umuhimu wa elimu msikimbilie maisha kila jambo lina wakati wake.”
Ziara hiyo ilienda sambamba na ukaguzi wa hali ya usafi wa mialo na kuongea na wavuvi na kuwafikishia taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu ambapo amewataka kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo yakienda sambamba na matumizi ya maji safi na salama kwa kuweka maji safi ya kunawa pamoja na sabuni na kuhakikisha wananchi wananawa ili kuweza kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.
Aidha Mhe Masala, amewataka Mama lishe kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo wanapopika vyakula vyao. Kwa kuchukua tahadhari kwani wasipokuwa makini unaweza kutokea mlipuko wa kipindupindu, huku akiwataka maafisa afya wafanye jitihada za kukagua maeneo mapishi yanafanyika na pindi watakapokuta mama lishe hakidhi vigezo vya kutoa huduma kufunga biashara zao kwani kwa kufanya hivyo ndio usalama wa wananchi/walaji.
“Mazingira lazima yawe masafi maji yanayotumika yawe masafi, majiko yawe masafi, kupunguza uwepo wa nzi na tule chakula ambacho ni cha moto”, alisistiza Mhe Masala.
“Ni wajibu wetu kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kama wana mwanza hivyo Kila mmoja awe mlinzi na msimamizi wa mwenzake, hili ni jukumu letu sote.”Alihitimisha.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.