Mhe. Hassan Masala, Mkuu wa wilaya ya Ilemela amewataka maafisa elimu watendaji, viongozi wa kata na mitaa kwa kushirikiana na wazazi, kufanya ufuatiliaji wa haraka kwa wanafunzi 1500 ambao hawajaripoti shule ili kuweza kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2023 wanaripoti shuleni.
Agizo hilo amelitoa wakati wa kikao kazi cha kutathimini hali ya uandikishaji wa darasa la awali na la kwanza na hali ya kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 ambapo amewataka viongozi na watendaji kushirikiana pamoja kuhakikisha watoto ambao hawajaripoti wanaripoti ndani ya wiki mbili.
Aidha Mhe Masala mbali na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha za ujenzi wa madarasa amekemea dhana potofu iliyojengeka kwa jamii kwamba hakuna sababu ya kusoma kwa kuwa ajira ni changamoto hivyo akatumia wakati huo kuwaasa wataalam na viongozi kutoa elimu kwa wazazi wasioelewa juu ya umuhimu wa elimu huku akihimiza kuwekeza katika elimu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe. Renatus Mulunga amempongeza Mhe Masala kwa kuendelea kuweka msisitizo juu ya suala la Elimu kwani anaamini maendeleo yoyote hupatikana kupitia elimu huku akihimiza kuwajali walimu wanaofanya kazi katika maeneo ya pembezoni kwa kuwaboreshea mazingira ya kuishi
Kwa upande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary ametaja mafanikio yaliyofikiwa kwa muda mfupi ndani ya sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya tano za sekondari, ujenzi wa shule saba mpya za msingi, pamoja na ukamilishaji wa maboma 40 ya vyumba vya madarasa yanayosubiria kupauliwa pamoja na kuahidi milioni tano kwa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka huu sambamba na kuwataka wenyeviti wa mitaa kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuboresha zaidi sekta hiyo.
Tathmini hiyo ilienda sambamba na utoaji wa vyeti kwa viongozi mbalimbali kwa ajili ya kutambua michango yao katika sekta ya Elimu, ambapo Mkuu wa Wilaya aliwatunuku vyeti hivyo, wenyeviti wa mitaa, watendaji kata na mitaa, wakuu wa shule , Mkurugenzi, Mstahiki Meya pamoja na Mbunge wa jimbo la Ilemela huku akiwashukuru kwa utayari wao katika kusimamia miradi ya elimu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.