Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala amekataza michango ya aina yeyote itakayosababisha wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2023 washindwe kuripoti shuleni.
Agizo hilo amelitoa leo wakati wa ziara yake kwa shule za msingi na sekondari ndani Manispaa ya Ilemela yenye lengo la kufuatilia mahudhurio ya kidato cha kwanza, awali na darasa la kwanza, kusikiliza changamoto za walimu na kuhamasisha ufaulu ambapo amewataka wakuu wa shule, maafisa elimu na viongozi wa mitaa na kata kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti mashuleni na kwamba hakuna kuzuia mtoto yeyote kuingia darasani
‘.. Kuna wazazi mnawazuia eti sababu hawajajaza fomu za kujiunga na shule kwenye kile kipengele cha daktari, wengine kwa kukosa sare, wengine sijui hawana jembe. Nasema marufuku kuzuia watoto kwasababu ya michango yeyote ..’ Amesema
Aidha Mhe Masala mbali na kumshukuru na kumpongeza Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa ujenzi wa madarasa, viti na meza ametaka kuchukuliwa hatua wazazi watakaoshindwa kupeleka watoto shuleni pamoja na watendaji watakaokwamisha zoezi la wanafunzi kuripoti shuleni.
Akimkaribisha mkuu huyo wa wilaya, Mwakilishi wa afisa elimu sekondari manispaa ya Ilemela Mwl Alex Mkusa amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha manispaa ya Ilemela inaendelea kushika nafasi nzuri kitaifa huku akiwataka kuongeza juhudi katika ufundishaji ili ufaulu kwa nafasi na daraja la ufaulu viende sambamba (GPA)
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mecco Mhe Godlisten Kisanga amewaasa viongozi wa mitaa kushirikiana kuhakikisha watoto wote wanaripoti shuleni sanjari na kuahidi ufuatiliaji wa nyumba kwa nyumba ili kubaini watoto waliochaguliwa na hawajaripoti mashuleni
Jumla ya wanafunzi 12,507 wamepangwa kuripoti shuleni kwa mwaka wa masomo wa 2023 ndani ya wilaya ya Ilemela ambapo mpaka sasa wanafunzi 6367 pekee ndio waliokwisha ripoti mashuleni sawa na asilimia 53 ya wanafunzi wote huku wanafunzi 6140 wakiwa hawajaripoti
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.