Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Mathias Severine Lalika amekabidhi jumla ya kadi 1200 za bima za afya iliyoboreshwa kwa wanachama wa chama cha madereva na makondakta mkoa wa Mwanza(MWAREDDA) pamoja na familia zao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mhe.Lalika amesema madereva na makondakta ni kundi linalopaswa kuheshimiwa katika jamii kwani shughuli wanazofanya zinawezesha watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka na ni shughuli inayochochea ukuaji wa uchumi kwa namna tofauti.
“Nawapongeza MWAREDDA kwa maamuzi mazuri waliochukua katika kujali usalama na afya zao lakini pia ni kitendo kinachounga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya Mhe .John Pombe Magufuli inayohamasisha wananchi wake kuwa na bima za afya ili wapate huduma hizo kwa haraka na ukamilifu pindi zinapohitajika bila kujali hali ya kifedha anayoweza kuwa nayo mwananchi kwa wakati husika”amesema .
Aidha Mhe.Lalika amewataka MWAREDDA na wananchi wengine kwa ujumla kutambua kwamba unapokuwa na kadi ya bima ya afya ni mkombozi kwako kwani una uhakika wa kupata matibabu muda wowote .
Nae mratibu wa mfuko wa iCHF wilaya ya Ilemela ndugu Leornard amefafanua kwa kina namna ambavyo mfuko unavyofanya kazi na kusema kuwa, malipo yake ni Shilingi elfu thelathini tu kwa mwaka kwa kaya ambayo itajumuisha wanafamilia sita.
“Huduma hii ni nafuu,tujiunge kwa wingi kwani uwingi wetu ndio maboresho ya huduma bora zaidi. Wanufaika wa TASAF , wanavikundi mbalimbali mnakaribishwa kujiunga na bima hii ya afya kwani ni msaada mkubwa kwetu, alisisitiza.
Nae Mwenyekiti wa chama cha madereva na makondakta Mwanza ndugu Mjarifu K.Manyasi amewapongeza wanachama wake kwa kujiunga ma bima ya afya iliyoboreshwa.
“Napongeza umoja wetu kwa ujumla kwani umekuwa wenye tija kubwa,nasisitiza umoja,mshikamano udumu ili tuendelee kupiga hatua kubwa zaidi.Tunakumbuka kwamba malengo ya umoja wetu ilikuwa ni kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii lakini sasa hivi tumeingia katika masuala ya afya”, Alisema
Akijibu changamoto ya madereva kutokuwa na mikataba ya kazi iliyotajwa katika risala ya MWAREDDA Mhe.Lalika amesema sheria ya nchi inataka watumishi wote kuwa na mikataba kwani ndio dira ya kazi mhusika anayokwenda kufanya.Mishahara ni lazima iendane na hali halisi ya maisha.
Aidha Mhe DC amewataka madereva kufata sheria na taratibu zilizowekwa bila shuruti katika kujiepusha na changamoto ya kutozwa faini za mara kwa mara pindi wawapo barabarani.
Pamoja na hayo, Mhe.Lalika ametoa tahadhari kwa wananchi wa Wilaya ya Ilemela kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Korona kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya,kunawa mikono na maji tiririka,kujiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na kuvaa barakoa katika maeneo ya mikusanyiko.
Jumla ya kaya 200 zenye jumla ya wanachama 1200 wa MWAREDDA zimekabidhiwa kadi leo, ambapo mchakato wa kupata bima za afya ulianza mwezi Juni baada ya wataalam wa afya wa manispaa ya Ilemela kuwaelimisha MWAREDDA na wao kupokea kwa vitendo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.