Katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela wakili Mariam Msengi amewataka wananchi wa Ilemela kuzingatia lishe bora katika ulaji wao wa kila siku huku akisisitiza umuhimu wa taifa kuwa na wananchi wenye afya nzuri katika kuijenga nchi.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya lishe katika mtaa wa Nyambiti uliopo kata ya Buzuruga wakili Msengi amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kuweka juhudi kubwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma bora za afya kwa kuimarisha miundo mbinu mbalimbali ya sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma hizo ndani ya Manispaa hiyo huku mkazo wa utoaji elimu ya lishe ukiendelea.
"...Kina mama sisi ndo viongozi wa familia katika mambo haya,tuwe mstari wa mbele kuzingatia lishe bora kwa familia zetu..."
Akitoa taarifa wakati wa maadhimisho hayo Afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasim amesema takwimu za mwaka 2023/2024 zinaonyesha asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa, asilimia 12 wana uzito pungufu na asilimia 3 wana ukondefu sambamba na hali duni kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (mwaka 15 - 49).
"...tunayo mafanikio tangu kuanzishwa kwa mpango wa lishe kitaifa ikiwemo kuongezeka kwa mwitikio wa jamii kuhudhuria elimu za lishe na kuleta watoto kupata nyongeza ya matone ya vitamin A na dawa za minyoo ambapo lengo lilikuwa watoto 66,381 na tukapata watoto 66,711 sawa na asilimia 100.4..." amesema Pili.
Nae diwani wa kata ya Buzuruga Mhe.Manusura Sadick Lusigalie amewataka wananchi wake kuunga mkono serikali ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia ulaji sahihi wa makundi yote muhimu ya vyakula ili kuleta nguvu kazi yenye matokeo chanya kwa taifa.
Scola Chacha ni mkazi wa mtaa wa Nyambiti yeye anashukuru wataalam hao kwa elimu walioipata na kuahidi kuwa balozi mzuri kwa wananchi wenzake.
Huduma zilizotolewa wakati wa maadhimisho hayo ni pamoja na kipimo cha HIV na sukari, chanjo mbalimbali kama polio,chanjo zote za watoto,matone ya vitamini A na dawa za minyoo na kipimo cha urefu na uzito wa mwili sambamba na jiko darasa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.