Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia wataalam wake wa mifugo wameendelea na uchanjaji wa kuku ikiwa ni awamu ya kwanza ya zoezi la uchanjaji wa mifugo, na utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kupunguza na kutokomeza vifo vya mifugo ambapo wafugaji wa kuku wameendelea kunufaika na chanjo hiyo ya kideri, ndui na mafua makali ya kuku inayoendelea kutolewa katika kata zao.
Wafugaji hao wa kuku katika nyakati tofauti wameishukuru serikali kwa kuleta chanjo hizi kwani kupitia ufugaji wamekuwa wakiongeza kipato chao huku wakitarajia kuwa kupitia chanjo hii kuku wataepukana na magonjwa.
“Huko nyuma nilikuwa nawatibu kuku wangu kwa njia ya kienyeji, walisumbuliwa sana na magonjwa na wengine walikufa lakini sasa hivi natarajia mifugo yangu itakuwa na afya njema kupitia hizi chanjo",Bw. Philipo Opati mkazi wa kata ya kahama
Naye kijana Yakobo Leonard, mtoto wa mfugaji wa kuku katika kata ya kahama amesema kuwa ufugaji wa kuku unawasaidia kuongeza kipato, chakula na kumuendeleza kielimu hivyo ameishukuru serikali kwa kutekeleza zoezi la utoaji wa chanjo kwani litasaidia afya ya mifugo yao kuimarika na pato la familia litakua.
Bi. Recho Thomas kamalambo mkazi wa kata ya Buswelu ambaye pia ni mfugaji wa kuku ameeleza kuwa kuku wake wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbali mbali na wengi wamefariki kwa kukosa maelekezo sahihi ila kwa sasa atazingatia maelekezo ya wataalam katika kuhakikisha mifugo yake inaepukana na mgonjwa.
Kwa upande wake Dkt. Nelson Rugemukamu, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela amebainisha kuwa tangu kuanza kwa zoezi hilo tarehe 03.07.2025 hadi sasa, kata 11 kati ya 19 za Manispaa ya Ilemela zimeshafikiwa na zoezi hili
“Hadi sasa kata 11 kati ya 19 zilizopo katika halmashauri yetu zimeshafikiwa na zoezi la utoaji wa chanjo ambalo litahitimishwa tarehe 14 Julai, 2025 hivyo nawasihi wafugaji muendelee kutoa ushirikiano kwa wataalam ili zoezi liweze kukamilika kwa mafanikio” Alisitiza Dkt. Nelson
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.