Waziri wa Afya Tanzania Mhe.Ummy Mwalimu (Mb) amezindua chanjo ya kansa ya mlango wa kizazi HPV (Human Papilloma Virus) kwa watoto wa umri kuanzia miaka 9-14 kitaifa katika viwanja vya Furahisha vilivyopo kata ya Kirumba ndani ya Manispaa ya Ilemela.
Mhe.Ummy amesema chanjo hii imefanyiwa majaribio kadhaa na wataalam kutoka wizara ya Afya na wadau wa kimataifa ikiwemo shirika la Afya duniani (WHO)kabla ya kuanza kutimika na kujihakikishia kuwa ni salama kwa wasichana wa umri huo.
"Dozi ya chanjo hii ni moja tu kwa maisha ya msichana, wazazi tuhamasike kuwaruhusu mabinti zetu kupata chanjo hii muhimu."
Ameongeza kusema kuwa, chanjo huokoa maisha,huwezesha taifa kuwa na nguvu kazi imara. Ametoa wito kwa wazazi wote wenye watoto chini ya miaka 2 kuwapatia chanjo zote kwa kufuata ratiba ya dozi iliyo sahihi.
Amefafanua kuwa virusi vya ugonjwa wa kansa ya mlango wa kizazi vinapatikana kwa wanaume na vinaweza kuingia kwa wasichana kupitia tendo la kujamiiana hivyo njia moja wapo ya kuepukana nayo ni kuacha kabisa kujihusisha na ngono katika umri mdogo.
"Tuwachanje mabinti zetu ili wasijeugua kansa ya mlango wa kizazi kwani ni hatari na pia matibabu yake ni gharama kubwa,tunasema hakuna saratani ya mlango wa kizazi Mwanza naTanzania kwa kuwapatia chanjo hii."
Mhe.Ummy amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa anayoendelea kuyafanya katika sekta ya afya kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za Afya na vifaa tiba.
Kwa Manispaa ya Ilemela takribani watoto 40,396 wanatarajiwa kupata chanjo hii chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa shule zote za msingi na sekondari kwa mabinti wenye umri wa miaka 9 hadi 14 kuanzia tarehe 22 hadi 28 Aprili,2024 .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.