Shule ya sekondari ya wavulana Bwiru imepongezwa kwa mipango, mikakati na juhudi ilizoweka na kufanikiwa kufuta alama sifuri katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2022
Pongezi hizo zimetolewa na meneja wa chuo cha elimu ya biashara tawi la Mwanza Bi Evelyne Manambo wakati wa sherehe za mahafali ya 83 ya kidato cha nne 2023 yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Bwiru wavulana ambapo ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kupata matokeo mazuri pamoja na kuwataka kuhakikisha wanafunzi wanaosoma shule hiyo wanapata daraja la tatu, la pili na la kwanza pekee katika matokeo ya miaka yote inakayofuata
‘.. Nipongeze kwa jitihada za kutokomeza sifuri, Tuhame kwenye kuondoa sifuri twende kwenye kuondoa daraja la nne, Kama huku tumeweza naamini na hili pia tutaliweza ..’ Alisema
Aidha Bi Manambo amepongeza nidhamu nzuri ya wanafunzi wa shule hiyo sanjari na kuwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi hao wanaendelea kuwa na nidhamu katika kipindi chote watakapokuwa nyumbani mara baada ya kumaliza mitihani yao wakisubiria kwenda hatua inayofuata
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni afisa elimu taaluma sekondari Mwalimu Alex Mkusa ameishukuru Serikali chini ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha kwaajili ya kurekebisha miundombinu ya shule hiyo pamoja na kumpongeza mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela kwa kutoa motisha ya milioni tano kwa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2022 huku akiwataka wazazi kulinda afya za wanafunzi katika kipindi chote watakapokuwa nyumbani
Nae mkuu wa shule ya Bwiru wavulana Mwalimu Thomas Werema akiwasilisha taarifa fupi ya shule hiyo amesema kuwa jumla ya wanafunzi 181 kati ya 211 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2020 wameshiriki mahafali ya 83 huku wengine wakishindwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, kuhama na kukariri darasa na kwamba shule ya Bwiru inakabiliwa na changamoto kuu mbili ambazo ni ukosefu wa vifaa vya kuhifadhia maji pamoja na mashine ya kudurufu huku changamoto nyenginezo Serikali inaendelea kuzitatua
Nazir Valentine ni miongoni mwa wahitimu wa kidato cha nne katika shule ya wavulana Bwiru mbali na kushukuru kwa kumaliza salama shule ameahidi matokeo mazuri katika mtihani wanaotarajia kuufanya hivi karibu sambamba na kuwaasa wanafunzi wenzake kwenda kuyaishi yale yote mazuri waliofundishwa wakati wakiwa shuleni
Katika mahafali hayo mgeni rasmi, meneja wa chuo cha CBE tawi la Mwanza ameahidi ununuzi wa mashine ya kudurufu na kuchapa yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni moja.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.