Wataalam na waheshimiwa madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba wamefanya ziara Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa lengo la kujifunza shughuli za ukusanyaji wa mapato na kuona namna ambavyo Manispaa ya Ilemela imekuwa ikifanikiwa katika shughuli zake mbalimbali za maendeleo hasa sekta ya uvuvi hali inayosababisha ukuaji wa kasi wa Manispaa hiyo.
Akisoma taarifa ya makusanyo ya vyanzo vya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025 Afisa mapato wa Halmashauri hiyo Theogenes Laurent amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 14.4 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2024 jumla ya shilingi Bilioni 13.6 zilikusanywa sawa na 94.8% ya lengo la bajeti huku Halmashauri hiyo ikipanga kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 14.9 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo mpaka sasa imekusanya 40.31% ya lengo kwa mwaka huu wa fedha.
Ivon Maha ni Afisa uvuvi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela amewaambia wageni hao kuwa uwekezaji mkubwa katika maeneo ya mialo unaweza kusaidia kuongeza mapato ya mazao ya uvuvi.
“..Manispaa ya Ilemela inashuhudia maendeleo makubwa ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi kwa kujenga na kuboresha miundombinu ambapo mialo inaendelea kuboreshwa,ujenzi wa viwanda vikubwa vinne vya kuchakata samaki na uanzishwaji wa viwanda vidogo 12 kwa ajili ya mazao ya uvuvi,vitalu nyumba vya kukaushia dagaa na masoko ya kisasa.” Amesema Maha
Ameongeza kuwa mafanikio katika sekta ya uvuvi yametokana na maboresho ya zana za uvuvi kama nyavu na boti sambamba na elimu ya matumizi yake kwa wavuvi,mikopo kwa ajili ya wavuvi inatolewa na utolewaji wa elimu ya ufugaji wa samaki kupitia mabwawa na vizimba shughuli ambayo imeongeza uzalishaji wa mazao ya samaki kwa matumizi ya majumbani na biashara.
“..Hongereni sana kwa kazi nzuri mnayoifanya,tuna vingi tumejifunza na ni lazima tuvifanyie kazi naomba mkurugenzi uridhie maombi yetu ya kuomba wataalam wako kuja kwetu kutuelekeza zaidi juu ya mengi tuliyoyaona hapa..”Amesema Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba Mhe.Privatus Mwoleka.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Neema Semwaiko amepokea pongezi nyingi zilizotolewa na wageni hao huku akikiri kuwa inatia moyo katika utendaji kazi na inachochea ari ya kufanya vizuri zaidi .
“..Halmashauri yetu ipo tayari kushirikiana na ninyi kwa namna ambavyo kwa pamoja tutaona inafaa na inaleta tija lengo ni kuhakikisha tunafanya kazi ili kuleta maendeleo kwa jamii zetu tunazozitumikia.”
Akihitimisha kusanyiko hilo Mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amesema ushirikiano ndio nguzo pekee katika kufanikisha mipango yote,ameongeza kuwa Manispaa ya Ilemela inafanya kazi kwa nguvu ya utatu ambapo yupo mbunge,serikali na wananchi.
“.. Halmashauri yoyote ili iendelee ni lazima kukusanya mapato,kikubwa ni elimu kutolewa kwa wahusika na sheria ziwepo na zisimamiwe kwa wale watakaokwenda tofauti wachukuliwe hatua..”
Maeneo yaliyotembelewa ni mwalo wa Kayenze ndogo uliopo kata ya Bugogwa na soko la samaki la kimataifa Kirumba ndani ya kata ya Kirumba.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.