Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 61.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya manispaa ya Ilemela katika sekta ya afya, elimu na miundo mbinu mbalimbali.
Hayo yamebainishwa na mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe. Renatus Mulunga wakati wa kikao cha baraza la madiwani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu inayoanza Januari hadi Machi, 2023.
Aidha Mhe.Mulunga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha hizo huku akilipongeza baraza la madiwani la Ilemela kwa kupata hati safi inayotokana na usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za maendeleo.
“ Naendelea kuishukuru Serikali kwa fedha inazoleta kutekeleza maendeleo, tuendelee kuwaombea viongozi wetu hasa Mhe Rais na Mbunge kwa juhudi zao za kuchochea maendeleo, Rais anatoa fedha nyingi sana katika miradi tunayotekeleza ..’ Alisema
Aidha Mhe Mulunga amemshukuru mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary kwa jitihada zake za ukusanyaji wa mapato zinazochochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuwataka madiwani kuunga mkono juhudi hizo
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary amefafanua kuwa mpaka sasa manispaa yake imeshakusanya kiasi cha shilingi 12,189,314,578 sawa na asilimia 90 ya makisio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kati ya mapato halisi ya shilingi 11,943,338,632 ambayo ni sawa na asilimia 92 ya bajeti.
Nae Diwani wa kata ya Pasiansi Mhe Rosemary Mayunga amempongeza mkurugenzi wa Ilemela na watumishi wote kwa mchango wao katika kuhakikisha manispaa hiyo inapata hati safi huku Diwani wa kata ya Mecco Mhe Godlisten Kisanga akisema kuwa hakuna manispaa inayopata hati safi kama kuna matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma hivyo kuwaasa wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo yao katika kutekeleza shughuli za maendeleo.
Manispaa ya Ilemela inaendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yake huku kukiwa na usimamizi wa matumizi sahihi wa fedha za miradi ya maendeleo kwa zaidi ya miaka kumi na kupata hati safi katika vipindi vyote.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.