Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia saba kukamilisha ujenzi wa Kivuko cha MV ILEMELA kitakachokuwa kinafanya safari zake Kutoka Kisiwa cha Bezi kuja Kayenze wilayani Ilemela ili kutatua adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano mheshimiwa Ashanta Nditiye wakati wa zoezi la uingizaji wa kivuko hicho majini, zoezi lililoendeshwa katika karakana ya Kampuni ya utengenezaji wa meli ya Ms Songoro Marine iliyopo kata ya Ilemela ambapo alisema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli imedhamiria kuimarisha sekta ya usafirishaji na kutatua adha mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa kutenga fedha kwaajili ya ujenzi wa vivuko 21 vipya na kukamilika kwa kivuko cha Mv Ilemela kinakamilisha idadi ya vivuko 31 nchi nzima kwa vipya na vya zamani.
‘.. Ndugu zangu Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni mbili nukta saba kuhakikisha kivuko hiki kinakamilika na mpaka sasa tumeambiwa zaidi ya asilimia 98 imeshakamilika na leo tunakiingiza majini kwa mara ya kwanza ...’ Alisema
Aidha kuhusu ajali mbalimbali zinazojitokeza nchini hasa ndani ya ziwa viktoria ameziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinazuia ajali hizo kwani zipo ambazo si za lazima zinazosababishwa na uzembe wa baadhi ya wataalamu wakiwemo madereva wasiokuwa na ujuzi wakutosha hivyo kuiagiza TASAC kufanya uchunguzi wa manahodha wa vyombo vya majini kabla ya kukabidhiwa vyombo vya usafiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe John Mongella aliishukuru Serikali na Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ndani ya mkoa wake ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, ujenzi wa Vivuko, ujenzi wa hospitali mpya mbili za wilaya ile ya Isanzu Ilemela na ya Buchosa, ukarabati wa hospitali ya mkoa Sekou Toure na ile ya rufaa ya Bugando huku akiwataka wananchi kuendelea kumuombea mheshimiwa Rais na kumuunga mkono.
Akihitimisha Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt. Angeline Mabula ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kumaliza adha ya usafiri ya muda mrefu iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa jimbo lake hasa wa maeneo ya Kayenze waliokuwa wakitaabika na suala la usafiri kwenda Kisiwa cha Bezi huku akiomba kuanza mapema kwa safari za kivuko hicho ili wananchi hao wasiendelee kuteseka sanjari na kuomba kupatiwa ufumbuzi kwa kero ya mawasiliano inayowakabili wananchi wa maeneo ya Sangabuye ombi ambalo lilipokelewa na naibu waziri wa uchukuzi na kumuagiza mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano kanda ya ziwa kushughulikia suala hilo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.