Takriban kiasi cha shilingi Bilioni 2.67 kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wilaya ya Ilemela katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yamebainishwa na meneja wa TARURA Wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya mpango wa matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika baraza la Madiwani la Manispaa ya Ilemela.
Mhandisi Sobe ameviainisha vyanzo vikuu vya fedha za matengenezo ya barabara katika utekelezaji wa kazi za matenegezo, ukarabati na ujenzi wa barabara kuwa ni mfuko wa matengenezo ya barabara, mfuko wa maendeleo ya barabara tozo na Jimbo. pamoja na wafadhili wengine kama Benki ya Dunia ambao hutekeleza miradi kwa kushirikiana na TARURA.
Kwa upande wa fedha za Mfuko wa Barabara amesema kuwa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.17 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara huku chanzo cha fedha za tozo kikiwa kimetengewa kiasi cha shilingi bilioni moja na chanzo cha mfuko wa jimbo kimetengewa kiasi cha Shilingi Milioni mia tano fedha hizo zikiwa ni kwa ajili ya matengenezo na ujenzi wa barabara katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ofisi ya TARURA Wilaya ya Ilemela imependekeza kujenga Barabara ya Kahama-Igogwe-Isanzu-Kabusungu (Ilemela Hospital road) 2.0km kwa kiwango cha lami nyepesi na barabara ya Mkudi (0.6km) kwa kiwango cha mawe kwa kutumia chanzo cha Mfuko wa Maendeleo ya Barabara na hii ni endapo tu bajeti hiyo itaridhiwa na kupitishwa katika ngazi za juu amesema Mhandisi Sobe
Wakichangia bajeti hiyo Waheshimiwa Madiwani wameshauri kuwa TARURA ijielekeze zaidi katika barabara ambazo zimekua korofi na zenye changamoto za muda mrefu hususani maeneo ya milimani ambapo wameshauri zijengwe barabara za mawe maeneo kama vile kitangiri,Kirumba,Nyamanoro na Ibungilo
“Jiografia ya Ilemela eneo kubwa imetawaliwa na milima, tujipange kwenye ujenzi wa barabara za mawe hasa maeneo ya miinuko kwani barabara za mawe ndio zinadumu kwa kipindi kirefu”, amesema Mhe Donald Ndalo diwani wa Kata ya Kitangiri akichangia bajeti hiyo.
Aidha waheshimiwa madiwani wameishauri TARURA kuwa, maeneo ya kuelekea kwenye taasisi kama vile zahanati,shule ,masoko na maeneo ya huduma za jamii barabara zake zifanyiwe matengenezo ya mara kwa mara.
Nae Mhandisi Sobe ameahidi ushirikiano na Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kujenga barabara ya kiwango cha lami kuelekea hospitali ya wilaya iliyopo Isanzu
Kwa mujibu wa takwimu za barabara zilizohakikiwa na wizara ya ujenzi, mtandao wa Barabara unaosimamiwa na TARURA Wilaya ya Ilemela una urefu wa km 875.85 Kati ya Mtandao mzima wa Barabara, Barabara za Lami ni km 37.16 sawa na (asilimia 4.24) Zege ni km 1.904(asilimia 0.22) Mawe Km 4.98 (asilimia 0.57) Changarawe ni km 92.03 (asilimia 10.51) na Udongo ni km 739.783 (84.46 asilimia).
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.