Shilingi Bilioni 13 inawezekana na itapatikana ni kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima alipokuwa akijitambulisha Ilemela kwa mara ya kwanza toka kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mhe Rais SamiaSuluhu Hassan huku akiwataka watumishi wa Ilemela kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato pamoja na kuwa wabunifu
Aidha Mhe. Malima amemuelekeza mchumi wa Manispaa ya Ilemel kuhakikisha anaweka mipango ya kufanikisha makusanyo ya fedha hizo yanawekwa wazi na yanakuwa shirikishi kwa kushirikisha idara zingine.
“Mapato ya mwaka jana ilikuwa Bilioni 9.6 na ilifikiwa na zidio kidogo na mwaka huu wa fedha malengo yenu ni Bilioni 13.5 naomba mipango ya kufanikisha makusanyo iwe wazi na ifanyike kwa ushirikiano na idara zingine kama timu.", Amesisitiza Mhe Malima.
Aliongeza kusema kuwa ni wajibu wake kutekeleza kile ambacho Mhe.Rais anategemea afanye kwa manufaa ya wana Mwanza na watanzania kwa ujumla kwani Kazi ya watumishi ni kuwahudumia wananchi na sio wao watuombe sisi.
Amesema , “Tutakaa mara kwa mara ili kujua kero na changamoto mbalimbali na kuweka mikakati inayotekelezeka ili kuungana na Mhe.Rais katika kutoa huduma bora na kuleta unafuu kwa wananchi."
Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa huyo ameitaka Ilemela kuwa ya mfano kwa halmashauri zingine kwa kuhakikisha masuala ya ulinzi na usalama yanaimarishwa zaidi ili kuifanya Ilemela kuwa sehemu ya kuvutia wawekezaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuongeza mapato ya Wilaya na taifa kwa ujumla
Ndugu Balandya Elikana, ambae ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza akijitambulisha amesisitiza suala la kufanya kazi kwa ushirikiano kama ndugu ili kuweza kutimiza malengo ya serikali huku akisisitiza kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu
“Ili kazi zetu ziende vizuri tunahitaji amani na kufanya kazi kwa ushirikiano kama ndugu, tufanye kazi ili kutimiza malengo ya serikali lakini pia tuwathibitishie waliotuamini kutupa majukumu haya ya kuhudumia wananchi kuwa tunatosha katika nafasi zetu.", Ndugu Balandya amesema
Mhe.Mkuu wa Mkoa umetukuta na zoezi la kampeni ya ujenzi wa madarasa na kuongeza madawati kwa ajili ya shule zetu za Ilemela naamini tutaendelea kushirikisha wananchi wetu katika kuleta chachu ya maendeleo zaidi Wilayani kwetu pamoja na hayo nikuahidi kuwa tupo tayari kumsaidia Mhe. Rais pamoja na wewe, alihitimisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hasan Masala.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.