Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imepokea jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 1,268,560,418.00 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari, Masemele sekondari katika kata ya Shibula na Kilabela sekondari katika kata ya Bugogwa pamoja na ujenzi wa nyumba moja ya walimu katika shule ya sekondari Kisenga iliyopo kata ya Kiseke.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli zilizotekelezwa na ofisi yake katika mkutano wa baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo amefafanua kuwa ujenzi wa kila shule utagharimu kiasi cha shilingi Milioni 584.2 sambamba na ujenzi wa nyumba moja kwa gharama ya shilingi Milioni 100 itakayogawanyishwa mara mbili “2 in 1” kwa ajili ya waalimu wawili kuishi.
“ Fedha hizi zilipokelewa mwishoni mwa mwaka wa fedha uliopita na taratibu za kutambua maeneo ujenzi utakakofanyika zinaendelea na tunatarajia utekelezaji wake utakamilika mara moja .”
Aidha Bi. Wayayu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya manispaa yake huku akiwaomba viongozi wenzake kuendelea kushirikiana katika kusimamia matumizi bora ya fedha hizo kwenye maeneo yao.
Nae Mbunge wa Ilemela Mhe.Dkt.Angeline Mabula mbali na kumpongeza Mkurugenzi huyo kwa taarifa nzuri ya utekelezaji amesema kuwa serikali kupitia ombi lake bungeni imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya ufundi itakayojengwa kata ya Bugogwa na shule mpya ya msingi itakayojengwa kata ya Shibula na kuwaomba madiwani kushirikiana katika maendeleo.
“ Wataalam wetu naomba muanze kuwaza ujenzi wa shule za ghorofa ,ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka .” Amesema mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga.
Diwani wa kata ya Nyakato Mhe.Jonathan Mkumba amepongeza taarifa ya Mkurugenzi iliyoonyesha mgawanyo mzuri wa fedha katika kila kata kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Sarah Shija ni mkazi wa mtaa wa Buswelu ni mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa baraza la madiwani yeye anapongeza jitihada za uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu inayofanywa na Manispaa .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.